Burkina Faso imepiga marufuku kituo cha televisheni cha Ufaransa TV5 Monde, ikikishtumu kwa kutoa "taarifa za kupotosha" kwa namna wanavyoangazia ugaidi nchini humo na katika nchi jirani ya Mali, mamlaka ya kuratibu vyombo vya habari imetangaza siku ya Jumanne.
TV5 Monde tayari matangazo yake yalishawahi kusimamishwa kwa muda mara mbili, Aprili na Juni 2024.
Baraza Kuu la Mawasiliano limefanya maamuzi yake ya sasa siku ya Jumanne, kupiga marufuku matangazo ya TV5 Monde katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Inafuatia "tathmini ya ukiukwaji wa sheria mara kadhaa, maadili na uwajibikaji kitaaluma katika kuangazia masuala ya kukabiliana na ugaidi" Burkina na kuhusu mashambulizi ya mwishoni mwa mwezi uliopita nchini Mali, mkuu wa baraza hilo Wendingoudi Louis Modeste Ouedraogo alisema katika taarifa.
'Taarifa za kupotosha, na kusifia ugaidi'
"Makosa yaliyofanyika, ambayo ni pamoja na taarifa za kupotosha na kusifia ugaidi, yamebainika katika matangazo kadhaa, kuanzia Aprili hadi Mei 2026," alisema.
TV5 Monde pia ilipigwa marufuku nchini Mali Mei mwaka uliopita kwa muda usiojulikana, baada ya serikali ya Mali kuishtumu kwa kukosa mizania kwenye kuangazia kwake maandamano ya upinzani.
Kilikuwa tayari kimesimamishwa kwa muda wa miezi mitatu mwaka uliotangulia.
















