| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Burkina Faso, Mali na Niger zimeanza rasmi mchakato wa kujiondoa ICC
Burkina Faso, Mali, na Niger zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mahakama hiyo imesema katika taarifa.
Burkina Faso, Mali na Niger zimeanza rasmi mchakato wa kujiondoa ICC
Burkina Faso, Mali, na Niger zimewasilisha rasmi notisi za kujiondoa kutoka ICC mnamo Septemba 2025. / Wengine / Others

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imethibitisha kuwa Burkina Faso, Mali na Niger zimewasilisha rasmi notisi za kujiondoa katika mahakama hiyo, hatua iliyoanzisha mchakato wa mwaka mmoja wa kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ICC, nchi hizo tatu za Afrika Magharibi zilitangaza mwezi Septemba 2025 kuwa zitaondoka katika mahakama hiyo, zikiituhumu kuwa ni "chombo cha ukandamizaji wa ukoloni mamboleo."

ICC ni mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi dhidi ya watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, pale ambapo mahakama za kitaifa zinashindwa au haziwezi kuchukua hatua.

Katika taarifa iliyochapishwa Jumatano, uongozi wa chombo kinachosimamia ICC ulithibitisha kupokea barua za kujiondoa kutoka Mali, Burkina Faso na Niger, hatua inayozindua rasmi kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kujiondoa kwao kukamilika.

CHANZO:Reuters