Waandamanaji nchini Libya Alhamisi wamevamia ofisi ya Umoja wa Mataifa iliyopo magharibi mwa mji mkuu Tripoli, wakipinga ripoti zinazodai kuwepo kwa mipango ya kuwahamisha wahamiaji nchini humo.
Video zilizosambazwa na wanaharakati kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha waandamanaji wakiingia ndani ya ofisi hizo katika eneo la Janzour, Tripoli.
Waandamanaji pia walifunga na kuweka vifusi vya mchanga katika lango kuu la ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi (UNHCR) katika wilaya ya Sarraj.
Katika taarifa, Shirika lisilio la Kiserikali la Al-Sarraj Social Council, lilitaka UNHCR iondoke nchini humo na kusitisha kile ilichokiita uungaji mkono kwa “wahamiaji haramu”.
Pia lilitaka serikali ya Libya iunge mkono juhudi za kuwafukuza “wavamizi” kutoka nchini humo.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa
Machafuko haya yalizuka baada ya ripoti za vyombo vya habari kudai kuwepo kwa mipango ya mashirika ya UN ya kuwapatia makazi mapya wahamiaji wasio na hati nchini Libya.
Hata hivyo, hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa serikali ya Libya wala Umoja wa Mataifa kuhusu madai hayo.
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya ilisisitiza kupinga mpango wowote wa kuwahamisha wahamiaji nchini humo.
Viongozi mbalimbali wa Libya, akiwemo mkuu wa Baraza la Taifa la Juu Mohamed Takala, mwanachama wa Baraza la ofisi ya rais Abdullah al-Lafi, na mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utawala Abdullah Qaderbouh, pia walikataa wazo la kuwahamisha wahamiaji wasio wa halali nchini humo.
Siku ya Jumanne, misheni ya UN nchini Libya ilionyesha wasiwasi wake kuhusu kile ilichokiita “kuongezeka kwa taarifa potofu na maneno ya uchochezi” dhidi ya wahamiaji.
Kuchochea mivutano
UNSMIL ilisema “habari kama hizi zinaweza kuongeza mvutano, kutoaminiana, ubaguzi na vurugu, na kuathiri heshima, usalama na maisha ya kila siku ya watu Libya”.
Siku hiyo hiyo, Naibu Kamanda wa vikosi vya mashariki mwa Libya, Saddam Haftar, aliamuru vyombo vya usalama kumaliza “uwepo usio halali” wa wahamiaji wasio na hati katika eneo la Libya.
Siku ya Jumatano, mamlaka za eneo la Zuwara magharibi mwa Libya zilitangaza amri ya muda ya kutotoka nje usiku kwa raia wa kigeni “ili kuimarisha usalama na utulivu wa umma”.
Uhamiaji usio rasmi unaendelea kuwa mkubwa kaskazini-magharibi mwa Libya, hasa katika maeneo ya pwani ya Mediterania kama Qarabulli, Sabratha na Zuwara, ambapo makundi hutumia mgawanyiko wa kisiasa na hali ya ukosefu wa usalama nchini humo.
























