Uhuru wa kusafiri na kurejesha heshima ya Mwafrika
Makubaliano ya Ghana na Zambia ya kuondoa viza kwa safari za raia wao yanatambua kuwa mzunguko huru wa watu ndiyo uti wa mgongo wa biashara, utamaduni, na kuchangamana kwa maarifa na fikra.
Rais John Dramani Mahama wa Ghana alipotembelea jiji la Lusaka, Zambia, katika ziara rasmi, kabla ya ziara hiyo makubaliano kadhaa tayari yamefikiwa: Ghana na Zambia zimekubaliana kufuta masharti ya viza kwa raia wa nchi hizo mbili.
Kwa mtazamo wa mtu mwenye jicho la kutilia shaka, hili linaweza kuonekana kama jambo dogo la kidiplomasia lisilo na uzito mkubwa. Lakini kwa mtazamo wangu, ni hatua ya kina, ya kimapinduzi, na yenye maana kubwa kisiasa. Hili si suala la kusafiri pekee; ni hatua muhimu dhidi ya moja ya urithi mbaya na wa kudhalilisha zaidi wa ukoloni barani Afrika: iliyounda tabia ya Waafrika kuwashuku Waafrika wenzawo.
Kwa miongo mingi, kikwazo kikubwa zaidi kwa wazo la Uanamajumui sio lugha, umbali, wala tofauti za kitamaduni, bali ni afisa wa uhamiaji katika viwanja vyetu vya ndege. Mara nyingi, la kwanza linalotokea kati ya mfanyabiashara mwanamke kutoka Ghana au msomi kutoka Zambia ni maswali ya kuchunguza, hali ya kutilia mashaka, na shaka ya kuwa wewe ni tishio —sio mshirika wa maendeleo.
Tulijenga vizuizi hivi vya kiurasimu kwa kisingizio cha usalama na mamlaka ya kitaifa, lakini tukaacha milango wazi kwa unyonyaji wa wageni. Kinaya chake ni kikubwa: mtalii kutoka Ulaya mara nyingi husafiri barani Afrika kwa urahisi zaidi kuliko mjasiriamali Mwafrika.
Tulibuni mfumo unaowachukulia ndugu zetu kama hatari, huku tukiwakaribisha kwa mikono miwili watu ambao kihistoria wamekuwa wakichota na kuondoa utajiri wetu.
Kujenga mitandao ya kiasili ya Kiafrika
Kwa muktadha huo, makubaliano ya Ghana na Zambia ni zaidi ya sera. Ni mabadiliko ya mtazamo wa kimsingi. Yanatangaza wazi kuwa raia wa Afrika si hatari wa kiusalama moja kwa moja. Yanakiri kuwa uhuru wa watu kusafiri ndiyo pumzi ya biashara, utamaduni, na maendeleo ya maarifa.
Fikiria athari zake: mbunifu wa teknolojia kutoka Accra anaweza kushirikiana bila vikwazo na mtaalamu wa nishati safi kutoka Lusaka. Mtayarishaji filamu kutoka Kitwe anaweza kuunda timu kutoka Tamale bila kupitia mateso ya kusubiri vibali vya kusafiri.
Hili ni suala la kujenga mitandao iliyo hai, imara, na huru—mitandao isiyohitaji ruhusa ya wale waliokuwa wakoloni wetu.
Hata hivyo, kuisifu hatua hii bila kuielewa historia yake ni kupunguza uzito wake wa kimapinduzi. Ghana na Zambia ni mataifa yaliyozaliwa kupitia mapambano makali dhidi ya ukoloni.
Kwame Nkrumah na Kenneth Kaunda hawakupigania uhuru ili vizazi vyao vijavyo vihitaji viza kubadilishana mawazo barani Afrika. Walitamani Afrika isiyo na mipaka, Afrika huru kwa maana halisi, ambako watu wake wangeweza kudai urithi wao wote bila vizuizi.
Kuondolewa kwa viza huku ni hatua ndogo lakini ya maana kuelekea kurejesha ndoto hiyo iliyoibwa. Ni kukataa ramani ya mgawanyiko iliyowekwa katika Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884—ramani ambayo tumekuwa tukiilinda sisi wenyewe kana kwamba ni ya kwetu.
Masharti ya kufanikisha ndoto hii
Mtihani halisi bado uko mbele. Kuondoa viza ni rahisi; kujenga mazingira ya kuufanya uhuru huo uwe na maana ndicho kibarua kikubwa zaidi.
Ni faida gani ya mipaka iliyo wazi ikiwa ni ngumu kubadilishana sarafu zetu wenyewe, njia za biashara ni duni, na masoko yetu yanajilinda dhidi ya Waafrika lakini yako wazi kwa bidhaa za kigeni zisizo na ushindani wa haki?
Hatua hii ya kidiplomasia lazima iwe cheche ya mabadiliko mapana zaidi:
1 - Ulinganifu wa mifumo ya kibiashara: Kutambuana kwa vyeti vya taaluma, kurahisisha usajili wa biashara, na mikataba ya kuepuka kodi mara mbili.
2- Uwekezaji katika muunganisho: Safari za anga, mifumo ya malipo ya kidijitali inayounganishwa, na mtandao wa intaneti wa kikanda unaopatikana kwa gharama nafuu.
3-Mabadiliko ya simulizi: Vyombo vya habari na mitaala ya elimu vianze kuthamini na kusherehekea mafanikio ya ushirikiano wa Waafrika kwa Waafrika, badala ya kuhalalisha tu Mataifa yalioendelea. Rais Mahama na Rais Hichilema wamebadilisha kanuni. Lakini kazi kubwa ni kubadilisha uhalisia.
Ndoto ya pasipoti ya Uanamajumui
Wameondoa kizuizi; sasa ni juu yetu kujenga ustawi uliopo nyuma ya lango hilo. Hili linahitaji kubadilisha dhana yetu ya usalama—kutoka kuzuia watu kuingia hadi kuujenga kupitia mshikamano, fursa, na ustawi wa pamoja.
Na hatua hii iwe mfano chanya unaoenea. Na ianze kuenea kutoka Ghana–Zambia hadi kila kona ya Afrika.
Siku ambayo Mwafrika ataamka Lagos, awe na mkutano wa mchana Nairobi, na kufanikisha ubia Johannesburg—kwa pasipoti moja na bila fedheha ya kiurasimu—tutakuwa tumeanza kujenga usanifu mpya wa heshima ya Mwafrika.
Hiyo ndiyo Afrika tuliyokusudiwa kuirithi. Na hiyo ndiyo Afrika ambayo ni lazima, kwa ujasiri na sera makini, hatimaye tuijenge.
Mwandishi, Kennedy Chileshe, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee Leaders Network, shirika la utetezi wa sera na uongozi.
Maoni ya mwandishi hayaakisi misimamo au sera za uhariri za TRT Afrika.