Naibu spika wa Bunge la Uganda Thomas Tayebwa ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kile anachokiita kuingilia mambo ya Uganda.
Hii ni baada ya Bunge la Ulaya kumuita balozi wa Uganda ili ajibu malalamiko yaliyotolewa kuhusu ghasia zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, 2026.
Tayebwa alikuwa akihutubia mkutano wa Kundi la Mabunge ya Kanda ya Afrika Mashariki la Umoja wa Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS-EU) unaonedelea Eswatini, kabla ya Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS–EU wiki hii.
"Moja ya masuala muhimu niliyosisitiza ni haja ya kudai heshima kwa nchi za Afrika kutoka kwa wenzetu wa Umoja wa Ulaya," alisema.
"Kwa mfano, Uganda hivi majuzi ilifanya Uchaguzi ambao ulikuwa huru na wa haki, na wenye mafanikio. Hata hivyo, Bunge la Ulaya lilimuita Balozi wa Uganda likimtaka kuelezea kuhusu uchaguzi huo; hii haikuwa sawa na tukaikataa.”
Naibu Spika pia alibainisha kuwa hii si mara ya kwanza kwa Umoja wa Ulaya kuingilia masuala ya ndani ya Uganda, akitolea mfano hali ya awali ambapo Bunge hilo hilo la Ulaya lilipitisha azimio la kutaka kusimamisha ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.
Mnamo Septemba 15, 2022, Bunge la Ulaya liliitaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Uganda na Tanzania kusitisha mradi wa ujenzi wa bomba hilo.
"Tulipinga vikali, na azimio hilo lilifutwa baadaye wakati wa mkutano wa Kundi la Mabunge ya Kanda ya Afrika Mashariki la Umoja wa Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki huko Maputo," Tayebwa aliongeza.
"Kama wabunge, ni lazima tuthibitishe jukumu letu la uangalizi ili kuhakikisha kwamba mikataba inaleta manufaa inayoonekana kwa raia wetu. Ni lazima tukuze kikamilifu Eneo Huria la Biashara la Bara la Afrika huku tukishughulikia vikwazo visivyo na ushuru ambavyo vinaendelea kuzuia upatikanaji wa masoko muhimu, na kushinikiza kuboreshwa kwa upatikanaji wa masoko ya Umoja wa Ulaya," alisema katika mkutano huo.


















