Rais Donald Trump siku ya Jumatano aliahidi kumpa kila raia wa Marekani mtu mzima $5,000 iwapo chama chake cha Republican kitaendelea kudhibiti mabunge yote mawili baada ya uchaguzi wa mwezi Novemba, akisisitiza ahadi hiyo ya kushangaza kwa kuwaambia wanaomuunga mkono "kufanya" kama wanamuona yeye anashiriki uchaguzi.
"Kama chama cha Republican kitashinda, na nyinyi mtashinda na kupata $5,000. Itaitwa takrima ya Trump ," aliwaambia wanachama wa Republican katika mkutano wa Dallas, huku chama hicho kikiwa nyuma katika kura za maoni ambazo chama cha Democrat kinatabiriwa kushinda.
Rais hakusema pale fedha hizo zitatoka -- huku gharama zikitarajiwa kuwa zaidi ya $1 trilioni -- akieleza kuwa "nchi yetu ina pesa nyingi sana."
Akisisitiza kuhusu kauli yake kuwa chama cha Republican kinaweza kupindua meza ya kura za maoni na kurudi kudhibiti mabunge yote mawili Novemba 3, Trump alisema "Nawaomba muone kama mnaniona mimi kwenye karatasi ya kupigia kura."
"Niko kwenye uchaguzi, niko kwenye uchaguzi -- kwa mara nyingine tena," aliuambia mkutano.
Kura za maoni zinaonesha uungwaji mkono wa Trump umeshuka kiwango cha 30, huku wapigaji kura wakiwa na hasira kuhusu gharama za maisha na vita walivyoanzisha dhidi ya Iran.
Shirika la takwimu za uchaguzi la Decision Desk HQ linatabiri kuwa chama cha Democrat kitashinda Baraza la Wawakilishi 230-205 na kuchukua udhibiti wa Seneti kwa 51-49 mwezi Novemba.


















