Kwa nini Kannywood inapambana kutafuta nafasi ya kuimarika ilhali Nollywood inaendelea kustawi
AFRIKA
5 dk kusoma
Kwa nini Kannywood inapambana kutafuta nafasi ya kuimarika ilhali Nollywood inaendelea kustawiSekta ya filamu ya Kihausa ya Kaskazini mwa Nigeria iko katika mgogoro, ikibanwa na uhaba wa sinema, udhibiti mkali wa kitamaduni na ufikiaji duni wa kidijitali.
Mipango mipya kama vile Arewaflix, jukwaa la kuonyesha filamu linalotoa manukuu ya lugha nyingi./ Wengine / Others
tokea masaa 16

“Unaweza kutengeneza filamu, lakini huna mahali pa kuipeleka.”

Wakati sekta ya filamu ya kusini mwa Nigeria (Nollywood) inasherehekea mapato makubwa ya sinema na mikataba yenye faida na majukwaa kama Netflix na Amazon Prime, hali ni tofauti kabisa kwa Kannywood. Kwa mujibu wa mkongwe wa Kannywood, Sani Mu’azu, hakuna kumbi za sinema kaskazini mwa Nigeria za kuonyesha filamu za Hausa.

Mu’azu—ambaye ni mtayarishaji, muongozaji, mwigizaji na rais wa zamani wa kitaifa wa Chama cha Watendaji wa Filamu Nigeria—ameitumikia Kannywood kwa zaidi ya miaka 30. Ameona ikikua kutoka mizizi ya kawaida hadi kuwa kitovu kinachozalisha mamia ya filamu kila mwaka. Lakini pia ameshuhudia sekta hiyo ikipoteza nguvu zake polepole, huku Nollywood ikiendelea kupiga hatua kubwa.

“Sinema inapaswa kukurudishia faida ya uwekezaji,” Mu’azu anaiambia TRT Afrika. “Kama huna skrini za kuonyesha filamu, huwezi kurudisha pesa zako. Ndiyo maana Kannywood haiwezi kumudu bajeti kubwa.”

Kwa miongo mingi, mazungumzo kuhusu filamu za Nigeria yamekuwa yakitawaliwa na Nollywood ya kusini—bajeti za mamilioni ya naira na maonesho makubwa ya kwanza jijini Lagos. Mbali na kelele hizo, Kannywood imekuwa ikipambana kuendelea kuishi dhidi ya udhibiti mkali, uharamia, ukosefu wa fedha, na misimamo mikali ya kitamaduni. Sasa inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi: jinsi ya kujiendeleza kidijitali na kufikia hadhira ya kimataifa bila kupoteza maadili ya kitamaduni yanayoitambulisha.

“Kannywood ni sehemu muhimu ya Nollywood,” anaeleza Mu’azu. “Nollywood ilianza kutoka sifuri hadi kuwa moja ya sekta kubwa zaidi za filamu duniani. Kannywood ilikuwa sehemu ya safari hiyo. Idadi ya filamu zinazozalishwa inaonyesha ni wabunifu wangapi wana hamu ya kusimulia hadithi zao.”

Kama Nollywood, Kannywood ilizaliwa kutokana na juhudi za watu wa kawaida, si msaada wa serikali. Watengenezaji wa awali walitegemea kanda za VHS, kisha VCD na DVD, zilizosambazwa katika masoko makubwa ya Kano kama Kofar Mata na Bata—sawa na Idumota na Alaba huko Lagos.

Lakini wakati Nollywood ya kusini ilipoboresha mbinu zake, ikaingia kwenye majukwaa ya kimataifa ya mtandaoni na kujenga sinema za kisasa (multiplexes), Kannywood ilikwama kwenye mifumo ya zamani.

Tofauti hiyo imezidi kuonekana wazi katika miaka ya hivi karibuni. Takwimu za Chama cha Waendeshaji Sinema Nigeria zinaonyesha kuwa sekta ya filamu nchini ilipata mapato ya naira bilioni 11.5 (takriban dola milioni 8.4) mwaka 2024—ongezeko la asilimia 60 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Ukuaji huo mkubwa ulitokea zaidi kusini, ambako kuna mamia ya skrini za sinema. Kaskazini mwa Nigeria, kwa kulinganisha, kuna sinema chache sana zinazofanya kazi, na zingine zimefungwa kabisa.

Pengo la kidijitali

Changamoto za Kannywood zinaonekana zaidi katika ulimwengu wa kidijitali. Wakati Netflix na Amazon Prime zinatoa nafasi kubwa kwa filamu za kusini mwa Nigeria, kuna maudhui chache sana ya lugha ya Hausa kwenye majukwaa hayo.

Kadri sinema zinavyoendelea kupungua na vikwazo vya maudhui vikizuia upatikanaji wa majukwaa ya OTT, wazalishaji wengi wa Kannywood wamegeukia YouTube. Hata hivyo, mapato huko yanategemea algorithimu badala ya mfumo thabiti wa usambazaji. Uharamia wa intaneti huko nao ni tatizo kubwa.

“Maharamia wanapakua na kusambaza filamu zetu na kupata pesa kidogo,” anasema Mu’azu. “Mtayarishaji hajui hata kwamba haki zake za uvumbuzi zinakiukwa na mtu mwingine anapata faida.”

Ingawa hadhira ya Kannywood ni kubwa sana—zaidi ya watu milioni 80 wanaozungumza Kihausa Afrika Magharibi, Kati na diaspora—idadi hiyo kubwa haimaanishi faida moja kwa moja.

“Wakazi wa kaskazini hawatumii intaneti kwa kiwango kikubwa kama maeneo mengine,” Mu’azu anaiambia TRT Afrika. “Na hata waliopo mtandaoni, wengi hawalipii kutazama maudhui.”

Miradi mipya kama Arewaflix, jukwaa la utiririshaji linalolenga kaskazini na kutoa manukuu ya lugha nyingi, inaonyesha ongezeko la uelewa kwamba Kannywood lazima ichukue hatima yake ya kidijitali mikononi mwake. Hata hivyo, Mu’azu anasisitiza uhalisia.

“Soko lipo,” anasema, “lakini upatikanaji wa intaneti kaskazini haukui kwa kasi kama ilivyo sehemu nyingine za nchi.”

Udhibiti wa serikali na usalama

Ili Kannywood ipige hatua, Mu’azu anaamini kuwa ushiriki wa serikali haukwepeki. Sera zitakazowafaidisha wawekezaji, msaada wa miundombinu ya sinema, mafunzo ya kitaaluma, na elimu ya kidijitali ni mambo muhimu.

Kwa upande mwingine, ukosefu wa usalama ni kikwazo kikubwa. Katika maeneo mengi ya kaskazini mwa Nigeria, vitisho vya utekaji nyara, uhalifu wa makundi yenye silaha, na mashambulizi ya kigaidi vimefanya uwekezaji wa burudani kuwa hatari sana.

“Hakuna mtu anayetaka kutazama filamu mahali ambapo kila mlango unafungwa saa kumi na mbili jioni,” anasema Mu’azu.

Ili utamaduni wa sinema uimarike, watazamaji lazima wajisikie salama kukusanyika maeneo ya umma. Lakini hali hiyo ya usalama mara nyingi haipo. Katika miji mingi, shughuli za kibiashara hupungua sana baada ya jioni, na matembezi ya burudani huonekana kama hatari zisizo za lazima.

Mwaka 2018, watu wenye silaha walishambulia sinema katika jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi, na kuua watu 11 huku zaidi ya 20 wakijeruhiwa.

“Tumejaribu kuvutia wawekezaji kutoka Lagos,” anasema Mu’azu. “Lakini ukosefu wa usalama unabaki kuwa tatizo. Unawezaje kuwekeza mahali ambapo hakuna uhakika wa chochote?”

Simulizi mpya

Licha ya changamoto zote, watengenezaji filamu wanaendelea kujaribu mitindo mipya—filamu za kihistoria, maudhui ya kijamii, na simulizi za kitaifa zinazovuka mipaka ya kikanda.

Filamu ijayo ya Mu’azu, Gamji Zone, imewekwa katika miaka ya 1960 na inaonyesha mapenzi kati ya mwanaume wa Kihausa na mwanamke wa Kifulani, yakitokea katika mazingira ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, utambulisho na utaifa, kupitia macho ya afisa Mwigbo.

“Si hadithi ya mapenzi tu,” anasema Mu’azu. “Filamu inahusu kuielewa Nigeria kama utamaduni mmoja licha ya tofauti zetu.”

Ikiwa kati ya kuendelea kuishi na kufikia ndoto kubwa, Kannywood sasa ipo kwenye njia panda—ikiwa na vipaji na mawazo mengi, lakini imefungwa na changamoto za kiuchumi, mapungufu ya sera, na uhalisia wa kitamaduni.

“Licha ya kuwa na uwezo mkubwa sana, Kannywood haijafika pale inapopaswa kuwa,” Mu’azu anaiambia TRT Afrika.

 

 

CHANZO:TRT Afrika