Somalia yapongeza uhusiano unaokua kati yake na Uturuki
AFRIKA
3 dk kusoma
Somalia yapongeza uhusiano unaokua kati yake na UturukiWaziri wa Somalia aliangazia nafasi ya Uturuki katika kujenga upya miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na bandari, barabara na vifaa vya uwanja wa ndege.
Somalia inapokea zaidi ya dola milioni 20 kutoka Uturuki kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi na shughuli za kidiplomasia. / / AA
23 Februari 2026

Waziri wa Bandari na Uchukuzi wa Somalia, Abdulkadir Mohamed Nur, amepuuza ukosoaji unaolenga ushirikiano kati ya Somalia na Uturuki, akilaani kile alichokiita upotoshaji kuhusu msaada wa Uturuki kwa taifa hilo la Pembe ya Afrika.

Waziri huyo alitetea nafasi ya Uturuki katika kuisaidia Somalia kujijenga upya na kuendeleza uchumi wake, akiielezea Uturuki kama mmoja wa washirika wa kuaminika na wenye manufaa makubwa kwa nchi hiyo.

Katika mahojiano maalum na TRT Afrika, Abdulkadir alisema kuwa Uturuki imejipatia shukrani za wananchi wa Somalia kupitia miaka ya misaada ya kibinadamu, uwekezaji katika miundombinu, na juhudi za kujenga uwezo wa taasisi mbalimbali.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa Uturuki nchini Somalia umejikita katika uwekezaji, ushirikiano wa kunufaishana, na uimarishaji wa uwezo wa taasisi — badala ya unyonyaji wa rasilimali.

“Mungu hakuwaumba wanadamu wote sawa,” waziri alisema, akibainisha kuwa wakati baadhi ya watu hutambua mema, wengine wanaweza kukosa shukrani. “Uturuki imejipatia shukrani. Wasomali waliosoma, wanaoelewa historia na kutazama mustakabali wa nchi yao, wanaelewa hili wazi.”

Abdulkadir aliangazia kuwa wakati dunia ilikuwa inapuuza Somalia, Uturuki ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kujitokeza kusaidia, hasa kufuatia ziara ya kihistoria ya Rais Recep Tayyip Erdogan mwaka 2011, alipokuwa Waziri Mkuu.

Waziri huyo alisifu Uturuki kwa kusaidia kuielekezea Somalia macho ya kimataifa kuhusu majanga ya kibinadamu, ikiwemo ukame na migogoro ya kivita.

Uwekezaji katika miundombinu na usalama

Abdulkadir aliangazia mchango wa Uturuki katika kujenga upya miundombinu muhimu kama bandari, barabara, na viwanja vya ndege. Alisema usimamizi wa bandari za Somalia na kampuni za Kituruki umeongeza kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali.

“Wakati kampuni za Kituruki ziliposimamia bandari za Somalia, mapato ya serikali yaliongezeka mara kumi,” alisema, akiongeza kuwa wakati huo Somalia haikuwa na utaalamu wa kiufundi wa kuendesha miundombinu hiyo kwa ufanisi.

Pia alitaja maboresho katika Uwanja wa Ndege wa Mogadishu, akisema kuwa hatua hizo zilirejesha imani kwa mashirika ya ndege ya kimataifa baada ya miaka ya changamoto za usalama na miundombinu. Maboresho ya vifaa na usalama, alisema, yamechangia kuongezeka kwa safari za ndege na kukuza uchumi kwa ujumla.

Waziri huyo alisema kuwa mamia ya mamilioni ya dola yanawekezwa kwa sasa katika sekta ya bahari ya Somalia — mtaji ambao serikali ya Somalia haina kwa sasa.

“Wawekezaji binafsi ndio wanalishughulukia swala hili,” alisema, akieleza kuwa makubaliano ya mgawanyo wa faida yatajadiliwa mara tu miradi itakapoanza kuzaa matunda, kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Alisisitiza kuwa kushiriki sehemu ya mapato katika mfumo unaokua ni bora kuliko kumiliki asilimia 100 ya rasilimali zisizoleta tija. “Kupata asilimia 30 yenye ukuaji ni bora kuliko kuwa na asilimia 100 ya sifuri,” alisema.

Uimarishaji wa uwezo na ushirikiano wa kijeshi

Abdulkadir alikiri kuwa Somalia kwa sasa haina meli, mifumo ya kiufundi, na utaalamu maalum unaohitajika kwa shughuli za kisasa za baharini. Alisema Uturuki imeisaidia kuziba mapengo hayo, ikiwemo kupitia ulinzi wa kijeshi wa shughuli za baharini.

Aidha, alisema Somalia inapokea zaidi ya dola milioni 20 kutoka Uturuki kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi na shughuli za kidiplomasia. Kulingana naye, michango hiyo inafadhiliwa na serikali ya Uturuki pamoja na wananchi wake.

“Hakuna jambo ambalo Uturuki inafanya na Somalia bila kuwa na lengo na dira ya baadaye,” alisema, akiongeza kuwa maarifa na ujuzi zinazotolewa na Uturuki zinaziwezesha kampuni za Somalia kuanza kuendesha shughuli kwa kujitegemea.

Akijibu wakosoaji wa ushirikiano huo, Abdulkadir alikanusha madai kuwa rasilimali za Somalia zinachotwa au kunyonywa.

“Somalia ni nchi inayojijenga upya. Huo ndio ukweli,” alisema. “Hatuna rasilimali zinazochimbwa na kusafirishwa nje ya nchi.”

Alisisitiza kuwa Uturuki haijachukua utajiri wa Somalia bali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo yake.

“Zaidi ya shukrani, hakuna lingine tunaweza kusema,” alihitimisha, akitoa wito wa kutumia “busara, akili, na fikra makini” katika kutathmini uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

 

 

CHANZO:TRT Afrika