Rais wa Uturuki asema msimamo “thabiti na wenye uwiano” wa kimataifa unaweza “kumzuia Netanyahu”
Recep Tayyip Erdogan asisitiza haja ya “shinikizo kubwa la kidiplomasia” dhidi ya Israel, na kusema kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yanapaswa kutekelezwa kikamilifu.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameisitiza jumuiya ya kimataifa kuchukua msimamo mkali na thabiti dhidi ya hatua za Israel huko Gaza, akibainisha umuhimu wa kuongeza shinikizo la kidiplomasia pamoja na kuhakikisha kufikishwa bila kukatizwa kwa misaada ya kibinadamu Gaza.
“Ninaamini kwamba jumuiya ya kimataifa ikionesha nia thabiti, endelevu na yenye uwezo wa kuweka vikwazo, inaweza kumzuia Netanyahu,” Erdogan alisema alipokuwa akirejea kutoka Johannesburg, Afrika Kusini, baada ya kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20.
Kuhusu ukiukaji wa Israel wa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, alisema Hamas “inaonyesha ustahimilivu mkubwa mbele ya uchokozi wote huu wa Israel na inazingatia usitishaji mapigano,” na kuongeza kwamba “utekelezaji kamili wa usitishaji huu wa mapigano ni muhimu.”
Kuhusu usalama wa eneo, rais huyo wa Uturuki alionya kwamba Ankara itachukua hatua madhubuti endapo itatishiwa. “Linapokuja suala la usalama wa taifa letu, kila mtu anajua hatua tulizochukua. Tukikumbana tena na hatari kama hiyo, tutafanya kinachohitajika.”
“Nguvu inayoinuka” katikati ya mabadiliko ya miungano ya kimataifa
Erdogan pia alisisitiza utayari wa nchi yake kusaidia upatanishi katika mzozo wa Urusi na Ukraine, akisema: “Kama Uturuki, jinsi tulivyochukua jukumu muhimu awali huko Istanbul, tuko tayari leo kudumisha msimamo huo huo wa kujenga.”
Akijibu maswali kuhusu pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump lenye vipengele 28 la kuleta amani Ukraine, alisema makubaliano yanaweza kupatikana ikiwa mpango huo utazingatia “matakwa halali na mahitaji ya kiusalama” ya pande zote mbili.
Aidha, Rais alisema Uturuki itaendeleza mwelekeo wake kama “nguvu inayoinuka” wakati miungano ya kimataifa ikibadilika. Alisisitiza uwekezaji katika teknolojia ya juu, nishati na ulinzi, ikiwemo uzalishaji wa ndani wa mizinga, ndege na mifumo ya ndege zisizo na rubani.
Kulinda muundo wa familia na kupanga sera “kwa kuzingatia miaka 50 hadi 100 ijayo” ni malengo ya msingi, aliongeza.
“Uturuki inalijenga taifa lake kwa mikono yake yenyewe,” Erdogan alisema. “Nchi tutakayokabidhi vizazi vijavyo itakuwa mbele sana kuliko ya leo.”