Watu saba, ikiwemo watalii sita na rubani, wamefariki siku ya Jumatano wakati helikopta ilipopata ajali eneo la Mlima Ololokwe kaskazini mwa Kenya, kulingana na vyombo vya habari vilivyowanukuu maafisa wa eneo hilo.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Ololokwe Kaunti ya Samburu, karibu kilomita 270 kaskazini mwa mji mkuu Nairobi.
Vyombo vya habari vya eneo hilo, vikinukuu maafisa, vimeripoti kuwa wote saba waliokuwemo kwenye helikopta walifariki. Bado uraia wa watalii hao sita haujabainika rasmi.
Mamlaka ya Kenya ya Safari za Anga (KCAA) imethibitisha kuwa haikuweza kutoa taarifa awali za watu wangapi waliofariki.
Helikopta zinatumika kwa ajili ya watalii
Mamlaka hazikueleza kuhusu chanzo cha ajali hiyo.
Maeneo ya Mlima Ololokwe, ambayo pia yanafahamika kama Ol Donyo Sabache, ni sehemu ya maeneo ya kitalii ya kaskazini mwa Kenya, ambayo hutembelewa na watalii wa kimataifa katika mbuga za eneo hilo.
Ndege ndogo na helikopta hutumika kwa ajili ya watalii kati ya hoteli wanazoishi na maeneo ya ndani ya hifadhi kaskazini mwa Kenya.
Kulingana na KCAA, wachunguzi wanajitahidi kutambua chanzo cha ajali hiyo.


















