Mwanamuiziki wa mtindo wa ‘Afrobeat’ Davido atakuwa miongoni mwa wanamuziki wakubwa watakao tumbuiza katika Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Huku viwanja vikiwa katika nchi ya Marekani, Mexico na Canada, muziki wa Afrika utarindima bila shaka.
Davido amechaguliwa kutumbuiza katika tamasha la Kombe la Dunia la FIFA Juni 10, 2026 huko Los Angeles, Marekani.
Atakuwa kwenye ukumbi wa Crypto.com pamoja na wasanii wa Marekani Major Lazer.
Katika taarifa yao Juni 2, FIFA ilisema tamasha hilo la Davido litakuwa na "shamra shamra kubwa" na watu "daima watakumbuka usiku huo wa muziki, soka na utamaduni".
Lakini midundo ya Afrika itaendelea zaidi.
Matamasha ya ufunguzi yatakuwa na wanamuziki wanaopendwa na Gen Z.
Mshindi wa tuzo ya Grammy, raia wa Afrika Kusini Tyla atakuwepo katika mji wa Mexico City Juni 11, kabla ya kuungana na mwanamuziki wa Afrobeat Rema siku ya pili katika uwanja wa SoFi huko Los Angeles kwa ufunguzi wa Marekani.
Hata hivyo, simulizi nzuri ni ile ya kundi la watoto kutoka Uganda, Ghetto Kids.
Wasanii hawa wadogo, ambao walianza safari yao katika kitongoji duni cha mji wa Kampala cha Katwe, wamefanikiwa kupata jukwaa kubwa zaidi.
Mwanamuziki maarufu duniani Shakira mwenyewe aliwaalika watoto hao kwa ajili ya tamasha la muda wa mapumziko la Kombe la Dunia New Jersey Julai 19.
Wataimba wimbo wa "Dai Dai," ambao ndiyo wimbo rasmi wa mashindano hayo akiwemo mshindi wa Grammy raia wa Nigeria Burna Boy. Shakira na Burna Boy pia watatumbuiza mjini Mexico City kwa moja kati ya matamasha matatu ya ufunguzi.













