Afisa habari wa Lebanon, mkewe wauawa katika shambulio lililofanywa na Israel
Miongoni mwa waliofariki wakati wa shambulio hilo ni pamoja na watoto na wajukuu wa wawili hao.
Afisa Habari wa Lebanon, pamoja na mke wake wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Israel siku ya Jumatatu, katika mji mkuu wa Beirut.
Kulingana na kituo cha televisheni cha Al-Manar, Mohammad Shari, ambaye pia ni Mkurugenzi wa vipindi vya siasa wa kituo hicho, na mkewe, waliuawa katika shambulizi hilo katika eneo la Zoqaq al-Blat, jijini Beirut.
Watoto na wajukuu wa wawili hao, pia walipoteza maisha katika shambulio hilo.
Jeshi la Israel limeongeza kasi ya mashambulizi ya anga nchini Lebanon katika siku za karibuni, dhidi ya Hezbollah, licha ya kuwepo na makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyoafikiwa mwezi Novemba, 2024.
Kulingana na mamlaka za Lebanon, watu wapatao 912 wamepoteza maisha na wengine 2,221 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel, kuanzia Machi 2.