Mwanasiasa wa Zambia mbaroni kwa 'picha iliyobadilishwa kidijitali' ya Rais Hichilema

Chapisho hilo kupitia mtandao wa Facebook linadaiwa kubadilishwa na kumuonesha Rais Hakainde Hichilema akiwa katika jeneza.

By
Mamlaka zimesema makosa yote ya kimtandao yanadaiwa kufanywa mjini Lusaka katika muda ambao haukutajwa. / Reuters

Katibu Mkuu wa chama cha National Democratic Congress (NDC) Mambwe Zimba inadaiwa amekamatwa mjini Lusaka kwa tuhuma za kubadilisha picha katika mtandao wa Facebook inayomuonesha Rais Hakainde Hichilema akiwa katika jeneza, vimeripoti vyombo vya habari za nchi hiyo.

Chapisho hilo kupitia mitandao ya kijamii linadai kuonesha picha iliyobadilishwa kupitia njia ya kidijitali ya rais akiwa katika jeneza, huku Makamu wa Rais Mutale Nalumango akionekana kutoa heshima ya mwisho, imeripoti Lusaka Times.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Wakala wa Uhalifu wa Mitandaoni wa Zambia umeanzisha uchunguzi siku ya Jumapili baada ya kupokea malalamiko kuhusu ukurasa huo wa Facebook unaoitwa "Zambia kwa wote 2026."

Mamlaka zimesema makosa yote ya kimtandao yanadaiwa kufanywa mjini Lusaka katika muda ambao haukutajwa.

Wachunguzi wa makosa ya mtandao walifuatilia madai hayo na kupelekea kukamatwa kwa Zimba mwenye umri wa miaka 44.

Polisi inaripotiwa pia kukamata simu aina ya Samsung A24 inayohusishwa na tukio hilo.

Uchunguzi wa awali inaonesha kwamba Zimba alikuwa miongoni mwa wanaoendesha ukurasa huo unaochunguzwa.

Polisi imewaambia waandishi wa habari kwamba picha hiyo haikupotosha tu bali pia ilikuwa na nia ya kuzua taharuki katika jamii.

Zimba hivi sasa anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Lusaka huku uchunguzi ukiendelea.

Mamlaka inasema kuwa uchunguzi utaendelea na kwamba kuna uwezekano wa wengine kukamatwa uchunguzi utakapokamilika.