Rais wa Ghana Mahama azua mjadala kwa kutumia ndege binafsi ya ndugu yake

Wakosoaji wanasema hatua hii inakiuka maadili ya maafisa wa umma na huenda ikasababisha "mgongano wa maslahi", lakini serikali inasema kuwa "inaokoa fedha za umma".

By
Ndege hiyo binafsi iliyozua mjadala inamilikiwa na mmoja wa wafanyabiashara matajiri nchini Ghana. Picha / GhanaWeb/X / Wengine

Wasiwasi umezuka nchini Ghana kutokana na safari za nje ya nchi za Rais John Mahama, ambazo anatumia ndege ya mdogo wake wa kiume.

Wanasiasa wa chama cha upinzani cha NPP wanataka kufanyike uchunguzi, huku mbunge Abdul Kabiru Tiah Mahama akisema hii inakiuka maadili ya maafisa wa umma na huenda ikasababisha "mgongano wa maslahi".

Hata hivyo, serikali imetetea uamuzi wa Mahama, kukanusha uwezekano wowote wa mgongano wa maslahi.

Waziri wa Nchi wa Mawasiliano wa Ghana, Felix Ofosu Kwakye, ameambia vyombo vya habari vya habari vya nchini humo, kuwa kwa Rais Mahama kutumia ndege ya ndugu yake "kunaokoa fedha za umma" kwa sababu serikali inalipia mafuta na ada ya kutua ndege.

Upinzani haijaridhishwa na maelezo haya.

Ndege ya Rais

Ndege ya rais wa Ghana, aina ya Falcon 900EX EASy, ilinunuliwa mwaka 2009. Imefanyiwa ukarabati wa miezi minane barani Ulaya na ilirudishwa Ghana Novemba mwaka jana.

Haifahamiki kama inaweza kutumika kwa sasa. Lakini Waziri Kwakye anasema "ndege ya rais imekuwa na matatizo mara kadhaa", kuzua wasiwasi kuhusu ubora wake iwapo rais ataitumia.

Hali hii ya sasa inakuja wakati Rais Mahama akifanya ziara Korea Kusini kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa mataifa mawili.

Pia amesafiri kwenda Ethiopia kwa mkutano wa Umoja wa Afrika, na Tanzania kuadhimisha miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

Ndugu yake Mahama, Ibrahim, ambaye ndege yake binafsi ndiyo inatumika, ni moja ya wafanyabiashara maarufu Afrika Magharibi, akiwa na biashara katika sekta ya madini, ujenzi, na kilimo.

Hivi karibuni alinunua ndege mpya na kuitoa nyingine itumike kama ‘‘ambulensi’’ kote nchini.