Kenya na Ethiopia vinara wa zao la maua

Wazalishaji hawa wakuu wa maua barani Afrika sasa wanakabiliwa na kushuka kwa kasi kwa biashara kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati.

By Coletta Wanjohi
Keny inaongoza barani Afrika kwa uzalishaji na mauzo ya nje ya maua / Reuters

Kenya na Ethiopia ni washiriki wakuu wa kimataifa katika uzalishaji wa maua yaliyokatwa, hii ikichangiwa na hali nzuri ya hewa nzuri ikiwemo kiangazi cha mwaka mzima.

Kenya inaorodheshwa kama muuzaji wa maua nje wa nne duniani ikiingiza zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 kila mwaka.

Ikiwa na zaidi ya mashamba 127 ya maua, Kenya imeorodheshwa baada ya Uholanzi, Colombia na Ecuador.

Kenya huchangia takriban asilimia 40 ya mahitaji ya maua katika masoko ya Ulaya na zaidi ya asilimia 15 kimataifa.

Mafanikio haya, yamechangiwa zaidi na uwepo wa usafirishaji wa ndege ikiwa ni pamoja na Shirika lake la Taifa la Kenya Airways.

Wataalamu wa kilimo hicho wanasema soko linaendelea kukua, na matarajio yao ni kufikia Dola bilioni 1.15 kwa mwaka 2026.

Kilimo cha maua kinasalia kuwa chanzo muhimu wa fedha za kigeni, kikiorodheshwa sambamba na chai, kahawa, na utalii, na kuchangia takriban  asilimia 18 ya mapato ya nje.

Ua maarufu zaidi ni waridi, likichukua zaidi ya asilimia 65 ya thamani ya mauzo ya nje, na kuongezeka kwa uzalishaji wa maua ya majira ya joto kama Limonium, Solidago na Hypericum.

Wakati Umoja wa Ulaya (EU) ukisalia kuwa soko kubwa zaidi, Kenya imepanua kikamilifu mauzo ya nje hadi Mashariki ya Kati hasa Dubai na China, na kupunguza utegemezi wa masoko ya jadi.

Kwa upande mwingine, Ethiopia ni muuzaji mkuu wa pili kwa ukubwa barani Afrika.

Ina uwezo wa kutoa maua yenye ubora wa hali ya juu mwaka mzima, na kukidhi mahitaji makubwa ya upanuzi katika eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba.

Kama ilivyo nchini Kenya, uuzaji wa maua nchini Ethiopia nao, unaongoza kuiingizia nchi hiyo fedha za kigeni, huku maua yakichangia zaidi ya asilimia 80 ya mapato yote ya mauzo ya nje ya kilimo cha bustani, ikifuatiwa na matunda na mboga.

Katika mwaka wa fedha wa 2024/25, nchi ilipata Dola milioni 564.9, ikisaidiwa zaidi na matumizi ya teknolojia ya kisasa, kukidhi viwango vya kimataifa, na kuboreshwa kwa upatikanaji wa soko.

Usafirishaji wa mwaka huo wa maua ulivutia zaidi ya $285M.

Mwezi Septemba na Oktoba 2025, Benki ya Taifa ya Ethiopia na Wizara ya Kilimo zilianzisha bei za juu zaidi kwa maua yaliyokatwa, ikijumuisha ongezeko la kati ya asilimia 7 hadi 11 kwa mashamba ya waridi, lililolenga kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Muundo mpya wa bei unaweka kiwango cha waridi kuwa Dola za Marekani 4.57 kwa kilo kwa mashamba ya nyanda za juu, Dola 4.76 kwa mashamba ya nyanda za kati, na Dola 5.12 kwa maeneo ya nyanda za chini.

Sekta hii inatofautiana zaidi ya waridi, ikilenga zaidi "maua ya kiangazi" kama vile majani ya Eucalyptus kama njia mbadala ya gharama nafuu.

Uholanzi, Saudi Arabia na Uingereza ndizo zinazoongoza kununua maua ya Ethiopia.

Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na mivutano ya kikabila, haswa katika maeneo yanayozalisha maua daima kumeathiri biashara.

Wazalishaji hawa wakuu wa maua barani Afrika sasa wanakabiliwa na kushuka kwa kasi kwa biashara kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati.

Kupungua kwa mahitaji pamoja na usumbufu wa usafirishaji hadi Mashariki ya Kati na Ulaya kwa mfano kumeshuhudia sekta ya kilimo cha maua nchini Kenya ikiripoti hasara ya hadi Dola milioni 1.4 kila wiki.

Nchini Ethiopia, wawekezaji wa sekta wanaripoti kushuka kwa asilimia 75 kwa mapato kwa baadhi ya mashamba yanayolenga masoko ya Ghuba