Frank Ilett: Nywele bado sinyoi
Nywele zako utanyoa lini? Bado zipo zipo sana, ndivyo ilivyo sasa kwa shabiki wa Manchester United Frank Ilett.
Shabiki huyu mwenye nywele nyingi aliweka nadhiri kuwa atanyoa nywele iwapo klabu anayoishabikia ya Manchester United itapata ushindi katika mechi tano mfululizo.
Aliweka nadhiri hiyo tarehe 5 Oktoba 2024, ambapo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kunyoa nywele zake na tangu wakati huo vijana wa Old Trafford hawajafanikiwa kushinda mechi tano mfululizo.
Kufikia mechi ya Jumanne usiku dhidi ya West Ham, Red Devils walikuwa wameshinda mechi nne na tayari Frank Ilett alikuwa ametia maji kichwa chake, ila maji yakazidi unga pale walipopata sare dhidi ya West Ham jijini London, na sasa Ilett ataendelea kusubiri ili atimize nadhiri yake.
Wakati Ilett akinyoa kwa mara ya mwisho 2024 alitaka watu wapige kura mtandaoni akiuliza swali unadhani nitanyoa 2024, 2025 au 2026?
Wengi waliopiga kura walikubaliana na 2026, bado mwaka mchanga sana na ana imani nywele zitanyolewa tu.
Yeye mwenyewe ana mashabiki zaidi ya milioni 2.3 kwenye mitandao ya kijamii. Pamoja na afro lake kuendelea kukuwa ikiwa sasa ni karibu siku 500 anasisitiza kuwa iwapo hakuna ushindi wa mechi tano, basi hakuna kunyoa.
Je, unaweza kuziacha nywele zako zikuwe kwa nadhiri ya timu unayoishabikia kushinda mechi ngapi?