Mamlaka nchini Kenya zimeutaka mtandao wa TikTok kuondoa maudhui ya kingono dhidi ya watoto, kama yalivyoripotiwa na Shirika la Habari la BBC.
Taarifa hiyo ya kiuchunguzi iliyochapishwa siku ya Jumatatu, inasema kuwa jukwaa la TikTok lilikuwa likipata faida kutokana na maudhui hayo yenye kuhusisha watoto wenye umri wa miaka 15.
Katika taarifa yake, Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imesema kuwa imeanza uchunguzi rasmi, huku ikisisitiza kuwa haitosita kutoa kuchukua hatua zozote dhidi ya mtandao huo wa nchini China.
Sheria za Kenya zinapiga marufuku manyanyaso ya watoto kwa njia mtandao.
Siku ya Jumanne, raia wa Uholanzi alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kusambaza picha za kingono za watoto kupitia mtandao wa WhatsApp.
Mtandao wa TikTok ndilo jukwaa la tatu kwa kuwa na wafuasi wengi, likitanguliwa na Facebook na WhatsApp.
Mtandao huo uliwahi kukumbwa na shutuma za kufanya upelelezi nchini Marekani, na kwa sasa uko chini ya uchunguzi wa Umoja wa Ulaya kwa madai kuwa ulikuwa na ushawishi katika uchaguzi wa Rais wa Romania.
















