Namna mjadala wa chuki dhidi ya Waislamu Uingereza unaonesha ubaguzi

Uingereza imetambua chuki dhidi ya Wayahudi (antisemitism) kama aina ya ubaguzi wa rangi kwa muda mrefu. Kwa nini basi, takriban muongo mmoja baadaye, chuki dhidi ya Waislamu bado inatumiwa kama mjadala wa kisiasa?

By
Maafisa wa usalama nje ya Msikiti wa East London, Agosti 2024, huku kukiwa na ongezeko la vitisho kwa jumuiya za Kiislamu kote Uingereza. /

Na Naomi Green

Kukabili kila aina ya ubaguzi kunamaanisha kuwatendea wanadamu wote kwa usawa na haki, si kuipa jamii moja upendeleo wa kipekee kuliko nyingine. Sera za umma lazima zizingatie usawa kwa wote.

Mnamo 2018, Kikundi cha Vyama Vyote Bungeni (APPG) kinachoshughulikia masuala ya Waislamu wa Uingereza, chombo cha wabunge na waheshimiwa kinachotoa ushauri bungeni, kilifanya mashauriano mapana na kutoa ufafanuzi wa kazi kuhusu chuki dhidi ya Waislamu (Islamofobia).

Ufafanuzi huu ulitambua chuki dhidi ya Waislamu kama aina ya ubaguzi wa rangi katika namna inavyojitokeza, ambapo Waislamu huchukuliwa kama kundi moja lenye sifa na tabia hasi zinazofanana.

Kwa kifupi, “Islamophobia” ni kuhukumu, kuwadharau, au kuwabagua Waislamu kwa misingi ya muonekano wao, mavazi, au utambulisho wao wa kidini.

Wanawake Waislamu mara nyingi hukumbana na vitisho na matusi katika maeneo ya umma, ikiwemo kwenye usafiri wa umma, mitaani, na madukani. Mashambulizi ya moja kwa moja yanayoripotiwa mara kwa mara ni kama kutemewwa mate, kusukumwa, kupigwa kibao, au kuvuliwa kwa nguvu mavazi yao kama vile hijabu.

 

Nguvu nyingi zimeelekezwa katika kupotosha hoja. Serikali iliunda kikundi kazi chini ya mwenyekiti Dominic Grieve KC, ambacho kilijaribu kuchanganya suala la “Islamofobia” na sheria za kukufuru au udhibiti wa uhuru wa kujieleza.

 Lakini ukweli ni kwamba: Islamofobia haina uhusiano wowote na mijadala ya kielimu ya dini. Ni kuwashambulia watu au makundi kwa misingi ya chuki au upendeleo hasi dhidi ya utambulisho wao wa Kiislamu, wa kweli au wa kudhaniwa.

Wapo wanaouliza kwa nini ufafanuzi unahitajika. Bila kufafanua jambo, huwezi kulitambua, kulifuatilia au kulikabili ipasavyo.

Ufafanuzi usio na nguvu ya kisheria pia ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na ubaguzi nje ya mfumo wa mahakama, kwa mfano kupitia elimu shuleni, ukaguzi wa usawa, na taratibu za ajira ili kuzuia chuki na ubaguzi kabla havijatokea.

Tangu ufafanuzi wa APPG upatikane, zaidi ya wasomi 800, makundi ya kijamii, wabunge, na serikali za mitaa wameuunga mkono. Kila chama kikuu cha siasa kilikubali ufafanuzi huu, isipokuwa Chama cha Conservative kilichokuwa madarakani wakati huo, ambacho kiliukataa na baadaye kumwondoa mshauri aliyeteuliwa kuandaa ufafanuzi mbadala.

Hivyo, ni jambo la kusikitisha kwamba baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2024, Chama cha Labour kiligeuka nyuma na kuacha msimamo wake wa awali wa kuunga mkono ufafanuzi wa APPG.

 

Machi mwaka huu, Mawaziri wa Labour waliunda Kikundi Huru cha Kazi, tena chini ya mwenyekiti Dominic Grieve KC pamoja na wataalamu wanne Waislamu, ili kupendekeza ufafanuzi mpya kwa ajili ya kutathminiwa. Kikundi hiki kilikabidhi mapendekezo yake mapema Oktoba, lakini hadi sasa serikali haijachapisha mapendekezo hayo wala kutoa majibu yake.

Wakati huohuo, watumishi wa umma wasiokuwa na mamlaka katika Wizara ya Makazi, Jamii na Serikali za Mitaa wanadaiwa kuvuja sehemu za mapendekezo hayo kwa vyombo vya habari vya mrengo wa kulia, na hivyo kuchochea wimbi la propaganda, upotoshaji na mijadala yenye nia mbaya katika wiki za karibuni.

Waislamu wa Uingereza wamezoea kuona viwango viwili katika siasa na vyombo vya habari, lakini wiki za karibuni zimekuwa na kiwango cha ajabu cha kupotosha ukweli na kupuuza hoja za msingi.

Chuki dhidi ya Waislamu imefikia viwango vya juu kabisa mwaka uliopita. Waislamu wametishwa na kushambuliwa; misikiti imelengwa katika matukio ya kigaidi, lakini habari hizi mara chache hupewa uzito katika kurasa za mbele. Vurugu dhidi ya Waislamu umeanza kuchukuliwa kama jambo la kawaida, hata katika vyombo vya habari vya kawaida.

Takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka ulioisha Machi 2025 zinaonyesha Waislamu wanaunda asilimia 45 ya uhalifu wote unaochochewa na chuki ya kidini, wakiwafuatiwa Wayahudi kwa asilimia 29.

Ukweli huu unaonesha wazi haja ya ufafanuzi bayana na rasmi kukubaliwa na serikali na jamii pana ya Uingereza.

Ukilinganisha na jinsi serikali ilivyokubali haraka ufafanuzi wa IHRA kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi (Antisemitism) mwaka 2016, ambao umekosolewa kwa kuchanganya ukosoaji wa Israel na chuki dhidi ya Wayahudi, swali linazidi kuwa muhimu: Ikiwa hilo liliwezekana ndani ya miezi michache, kwa nini “Islamofobia” imeachwa bila ufafanuzi kwa karibu muongo mzima?

Jaribio rahisi la kupima unafiki huu ni kujaribu kubadili neno “Uislamu” kwenye kauli fulani na kuweka dini nyingine.

Hivyo ndivyo vichwa vya habari na kauli zifuatazo zilivyoonekana katika vyombo vya habari na mijadala ya kisiasa:

1. “Uislamu umekuwa tatizo Uingereza kwa muda mrefu. Ni wakati wa kukabiliana nalo.”

2. “Uislamu wa kisiasa ni tatizo linalokua nchini.”

3. “Mpango wa serikali wa kufafanua ‘Islamofobia’ utazidisha mgawanyiko katika jamii.” 

4. “Kufafanua Islamofobia ni jambo la kijinga.” 

5. “Ufafanuzi wa Islamofobia hauhitajiki kwa kuwa Waislamu tayari wanalindwa kisheria.”

6. “Serikali ikisonga mbele na ufafanuzi wa Islamofobia, unapaswa kupitia mashauriano ya wazi ya umma kutathmini hatari na faida.” 

7. “Ufafanuzi wa Islamofobia unahatarisha kudhoofisha sheria za kupambana na ugaidi.”

8. “Labour yashusha ufafanuzi wa Islamofobia kwa hofu ya kudhibiti uhuru wa kujieleza.”

9. “Uharibifu wa tuhuma za ‘Islamofobia’.”

10. “Wanaounga mkono ufafanuzi rasmi wa Islamofobia wanataka kuutumia kuathiri sera za kupambana na ugaidi na sera za kigeni.”

 Jaribu kuyasoma upya ukiweka maneno “Uyahudi” au “Usikh” mahali pa “Uislamu”, ungeona haraka jinsi ambavyo kauli hizi zingekuwa zisizokubalika. Lakini zinapolengwa kwa Waislamu, mara nyingi zinachukuliwa tu kama mjadala wa kawaida.

Sasa Serikali inapaswa kuchukua hatua kwa uwazi, kwa kuchapisha kwa ukamilifu mapendekezo ya Kikundi Huru cha Kazi. Katika kelele zote za siasa na taarifa potofu, jambo la msingi limesahaulika: usalama wa jamii na usawa, si malumbano ya kisiasa au simulizi za vyombo vya habari.

Mpaka pale Islamofobia itakapokubalika na kuelezwa kwa uzito sawa na aina nyingine za ubaguzi wa rangi, Uingereza itaendelea kuhubiri usawa huku ikitekeleza viwango viwili.