Mkuu wa Jeshi la Iran atishia kujibu 'vitisho' vya Trump na Netanyahu
Maandamano yaliyosababishwa na ugumu wa maisha nchini Iran yanafuatiliwa kwa karibu na jamii ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na viongozi mahasimu wa taifa hilo, Israel na Marekani.
Kiongozi wa kijeshi wa Iran alionya kwamba Iran haitakaa kimya, baada ya Marekani na Israel kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali.
"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukulia kuongezeka kwa kauli za uhasama dhidi ya taifa la Iran kuwa tishio na haitavumilia kuendelea kwake bila kujibu," alisema Jenerali Amir Hatami, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars siku ya Jumatano.
Hatami, kamanda wa jeshi la Iran, alionya kwamba "ikiwa adui atafanya kosa" mwitikio wa Iran utakuwa mkali zaidi kuliko ule wa wakati wa vita vya siku 12 dhidi ya Israel mwezi Juni 2025.
Hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuingilia kati iwapo Iran itauwa waandamanaji, wakati huo huo Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel ameonyesha kuunga mkono maandamano hayo.
Tarehe 28 Disemba wafanyabiashara mjini Tehran walifanya maandamano kupinga ongezeko la bei na kuanguka kwa sarafu ya nchi hiyo rial, jambo lililosababisha maandamano kama hayo kufanyika katika miji kadhaa.
Maandamano hayo bado hayajakuwa makubwa kama yale ya mwaka 2022 hadi 2023, au yale ya 2009 yaliyojitokeza baada ya uchaguzi wa urais.
Lakini maandamano ya kiuchumi yamevutia jumuia ya kimataifa, ikiwemo kutoka kwa viongozi wa mataifa ambayo hayana uhusiano mzuri na Iran.
"Tunaangalia kwa makini sana. Ikiwa wataanza kuua watu kama walivyofanya zamani, nadhani watashambuliwa vikali na Marekani," Trump aliwaambia waandishi wa habari Jumapili.
Netanyahu, kwa upande mwingine, alisema mbele ya baraza la mawaziri la Israel: "Tunaungana kwa mshikamano na watu wa Iran na matarajio yao ya uhuru, uhuru binafsi na haki."
Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilimshutumu Trump na Netanyahu kwa kuhamasisha vurugu na kujaribu kuharibu umoja wa kitaifa wa Iran.