Kwa nini uhusiano wa Uturuki na Ethiopia wa miaka 100 ni muhimu
Huku uhasama kati ya mataifa ukiongezeka katika ushoroba wa Bahari ya Shamu, ziara ya Erdogan nchini Ethiopia inadhihirisha nafasi ya Uturuki katika kuelekeza uthabiti, usalama wa baharini na kuweka hali ya usawa katika kanda.
Na Esra Karataş Alpay
Ziara rasmi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, inadhihirisha uhusiano wa kidiplomasia wa zaidi ya karne moja.
Unajiri wakati ambao Pembe ya Afrika iko kwenye mgogoro wa bahari, ushindani wa mataifa yenye uwezo na kubadilika kwa mtazamo wa dunia.
Akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, makubaliano mapya yalitiwa saini katika sekta ya biashara, masuala ya angani, teknolojia na ushirikiano wa maendeleo.
Ilhali zaidi ya hafla hiyo rasmi, wachambuzi kutoka Uturuki na Ethiopia wanaeleza ziara hii kuwa na uzito mkubwa zaidi kikanda na duniani.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Rais Erdogan alisisitiza kuhusu vipaumbele vya Uturuki.
“Hatutaki mapigano mengine yaongezwe kwa madhila na hali ya kukosa usalama iliopo katika kanda kwa sasa,” rais alisema.
“Tunaamini kuwa Pembe ya Afrika haitakiwi kugeuzwa kuwa uwanja wa vita wa mataifa ya nje.”
Pia alisisitiza kuwa kwa Israel kutambua Somaliland hakutamfaidi mtu yoyote katika kanda nzima — matamshi yaliyoashirika msimamo wa muda mrefu wa Uturuki kuunga mkono uhuru wa mipaka ya Somalia.
Profesa wa ushirikiano wa kimataifa Suay Nilhan Acikalin kutoka Chuo Kikuu cha Haci Bayram Veli University jijini Ankara ameiambia TRT World kuwa karne moja ya uhusiano rasmi — ulioanza 1926, wakati Uturuki ilipoanzisha ubalozi wake wa kwanza nchini Ethiopia — inadhihirisha ngazi nyingi za ushirikiano zaidi.
“Hii karne ni ishara nzuri,” Acikalin alisema. “Lakini uhusiano umeanza zamani sana — kihistoria, kitamaduni na kijamii. Tunachokiona leo katika makubaliano ya kiuchumi na kidiplomasia yameweka katika msingi thabiti.”
Anasema umuhimu wa Ethiopia kutokana na idadi ya watu wake na eneo lake — ina idadi ya watu milioni 130 na iko karibu na Bahari ya Shamu — jambo linaloimarisha umuhimu wao.
“Ushirikiano huu ni zaidi ya mataifa mawili tu,” Acikalin anasema. “Una uwezo wa kuwa na ushawishi wa kuleta uthabiti katika Pembe ya Afrika na hata usalama wa baharini.”
Uhusiano wa kitamaduni na kihistoria
Profesa wa Ethiopia Yonas Adaye Adeto kutoka Chuo Kikuu cha Addis Ababa anatoa mtazamo mwingine, akisisitiza kuhusu ushirikiano wa karne nzima wa kitamaduni kati ya mataifa hayo mawili.
“Kihistoria, wote Uturuki na Ethiopia wamekuwa na ushawishi katika maeneo kadhaa kimkakati,” Adeto aliiambia TRT World. “na uhusiano wetu ni wa zamani zaidi miaka mia tano au mia sita iliopita, siyo tu miaka 100. Miaka hii 100 ni ishara tu.
Alieleza kuhusu mji wa kihistoria wa Harar, ambapo familia nyingi kitovu chake ni enzi za Ottoman.
“Tuna watu wengi Harar ambao wanadai asili yao ni kutoka Uturuki — na kweli ni hivyo,” Adeto says.
“Kwa hiyo hii siyo diplomasia tu, siyo suala la kiuchumi tu. Kuna msingi wa kitamaduni, wa kijamii zaidi ya upeo wa macho.”
Kwa Adeto, ziara ya Rais Erdogan inatoa ujumbe wa zaidi ya mataifa hayo mawili.
“Inatuma ujumbe kwa bara zima la Afrika — na ningesema kwa usalama duniani — kwamba Uturuki inakuwa na nafasi muhimu katika kanda hii yenye machafuko,” amesema.
Ameelezea Pembe ya Afrika na ushoroba wa Bahari ya Shamu kuwa sehemu ya vurugu kwa mataifa yenye uwezo kuanzisha kambi za kijeshi na kuangazia maslahi yao ya kimkakati.
“Nchini Djibouti na maeneo ya Bahari ya Shamu, kuna mkusanyiko wa nchi zenye uwezo katika karne ya 21,” amesema. “Kwa muktadha huu, ziara hii siyo tu inaadhimisha miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia lakini pia ishara ya amani — ni kama ziara ya amani.”
Adeto alieleza kuhusu mafanikio ya Uturuki katika nafasi ya upatanishi 2024, wakati uhasama kati ya Ethiopia na Somalia ulipozidi.
“Ni Uturuki ndiyo iliyoleta suluhu ya amani eneo hilo, na kurudisha uhusiano mzuri,” alisema. “Hali ilibadilika. Vurugu zikatulia.”
Mwanachuoni wa sayansi ya siasa na uhusiano wa kimataifa Serhat Orakci, kutoka Chuo Kikuu cha Halic jijini Istanbul, ameiambia TRT World kuwa ziara hiyo inaongeza mashindano katika eneo hilo.
“Itakuwa kosa kusahau China, UAE na Israel ambao wanataka kupanua ushawishi wao katika eneo hilo,” anasema. “Pembe ya Afrika imekuwa sehemu muhimu ya ushoroba wa bahari na kimkakati.”
Kwa Israel kutambua ‘Somaliland’, anaeleza, kumeibua mtafaruku mwingine.
“Kwa kutambua huko, uhuru wa mipaka wa Somalia unaonekana kutatizwa zaidi,” Orakci anasema. “Kwa hiyo msimamo wa Ethiopia umekuwa muhimu sana.”
Mwaka uliopita, Ethiopia ilitia saini makubaliano na ‘Somaliland’ ya kufikia Ghuba ya Aden — jambo lililozidisha uhasama na Somalia.
“Iwapo Addis Ababa itafuata nyayo za Israel au kuangalia upya mtazamo kwa lengo la kimkakati zaidi,” Orakci anaongeza.
Uturuki, ambayo imewekeza sana nchini Somalia tangu 2011 na kuwa na jukumu la upatanishi kati ya Somalia na Ethiopia, inataka uthabiti katika kanda na kuheshimiwa kwa uhuru wa mipaka ya Somalia.
“Ziara ya Rais Erdogan imejiri wakati muafaka,” Orakci ameiambia TRT World.
“Ushirikiano wa dhati kati ya Uturuki na Ethiopia — na kwa Ethiopia kuunga mkono msimamo wa Uturuki katika kanda — utakuwa muhimu sana.”
‘Uthabiti unahitaji usawa wa uhuru’
Profesa Adeto anaeleza kuhusu nafasi ya Uturuki katika suala pana la majadiliano duniani, kuhusisha na mijadala inayoendelea kwa sasa na mtazamo tofauti kimataifa.
Anasema kwa sasa usalama kote duniani unatetereka, akieleza kuhusu kile ambacho mataifa ya BRICS, nchi zenye uchumi wa chini duniani, na mataifa ya Afrika wanachotaka kuwa na nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kwa maoni yake, mfumo wa sasa wa kimataifa haufanyi tena kazi kwa uthabiti na unakuwa butu katika maeneo mengi.
“Ili kusawazisha hili, usawa wa uhusiano wa kimataifa, mifumo ya uhusiano lazima iimarishwe — na Uturuki inaibuka kama msawazishaji barani Afrika na mdau mwenye tija duniani.”
Pia alisisitiza kuwa lengo la Ethiopia kufikia bahari ni suala la kimkakati, akipendekeza kuwa Uturuki inaweza kuwa na nafasi muhimu ya upatanishi kuhakikisha kuwa malengo haya yanatimia kwa amani.
Profesa Adeto anaeleza kuwa elimu na uhusiano wa mtu kwa mtu, hasa ikizingatiwa kuwa karibu wanafunzi 60,000 kutoka bara la Afrika kwa sasa wanasoma nchini Uturuki.
“Mitazamo hii ya kiutamaduni na kielimu lazima iendelezwe zaidi,” anasema, akiangazia Dira ya 2063 ya Umoja wa Afrika. “Kwa malengo ya Afrika ya muda mrefu kufanikiwa, tunahitaji majadiliano chanya na yenye tija.”
Acikalin anakubaliana na hayo, akieleza kuwa ushirikiano unaolenga maendeleo unaenda sanjari na diplomasia inayojikita katika suala zima la amani.
“Pembe ya Afrika haitakiwi kuwa sehemu ya kufanyiwa masihara kwa mahasimu kutoka nje,” anasema. “Uthabiti wa kudumu unahitaji majadiliano ya usawa na yenye tija.”