Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema Jumanne kuwa ameagiza kufanyika kwa operesheni ya kusafisha maeneo ya manispaa yenye hatari kubwa na kuchukua hatua kali dhidi ya matumizi mabaya ya pombe ili kuwalinda wanawake, kufuatia mfululizo wa mauaji uliosababisha malalamiko na hasira nchi nzima.
Kupatikana wa miili ya wanawake 11 iliyotupwa katika eneo la Ekurhuleni, mashariki mwa Johannesburg, tangu katikati mwa Julai, umeibua tena wasiwasi kuhusu viwango vya juu vinavyoendelea vya ukatili wa kijinsia nchini.
“Taifa la Afrika Kusini limekasirika. Wanawake wa Afrika Kusini wamekasirika. Hasira yao ina msingi wa kueleweka. Nami pia nimekasirika,” Ramaphosa alisema katika hotuba ya kitaifa.
Alisema serikali imeanzisha operesheni ya dharura ya kitaifa inayohusisha wataalamu kutoka nyanja mbalimbali ili kuchunguza mauaji hayo ya Ekurhuleni. Watu wanne walikuwa chini ya ulinzi wa polisi kuhusiana na tukio hilo.
“Kumekuwa na hofu kubwa kwamba kugunduliwa kwa miili ya wanawake hao katika maeneo yaliyo karibu kunaweza kuashiria kwamba mauaji hayo yalifanywa na mhusika mmoja,” Ramaphosa alisema.
“Hata hivyo, kwa sasa polisi hawajapata ushahidi unaothibitisha kwamba mauaji hayo yalifanywa na mhusika mmoja.”
Mwili wa mwisho ulipatikana Jumapili katika eneo la wazi. Siku moja kabla yake, mwili wa mwanamke aliyekuwa karibu bila nguo ulipatikana karibu na makaburi katika manispaa hiyo hiyo.
Maafa ya kitaifa
Waathiriwa wengi walikuwa katika umri wa miaka ya 20 na 30. Baadhi yao walikuwa wamevuliwa nguo na walionyesha dalili za kufanyiwa unyanyasaji wa kingono.
Ingawa ukatili wa kijinsia ulitangazwa kuwa janga la kitaifa mwaka jana, Ramaphosa alisema serikali imeshindwa kuwakinga wanawake ipasavyo. Alitangaza hatua mpya kadhaa za serikali, zikiwa na muda maalumu wa utekelezaji.
“Ni lazima tukabiliane na ukweli. Tulichofanya hadi sasa hakijatosha. Tunahitaji kufanya mengi zaidi,” alisema.
“Ni lazima kila manispaa ianze mara moja kuimarisha usalama wa wanawake,” alisema. “Maeneo hatarishi lazima yatambuliwe” na kuchukuliwa hatua.
Alisema ukaguzi huo unapaswa kubaini taa za barabarani zilizoharibika, maeneo ya umma yaliyoota nyasi na vichaka kupita kiasi, majengo yaliyotelekezwa, njia na vituo vya usafiri visivyo salama, bustani zisizolindwa vya kutosha, pamoja na hali nyingine zinazowaweka wanawake katika hatari.
Pia aliamuru kutekelezwa kwa “mpango wa utekelezaji wa sheria” wenye lengo la kupunguza vurugu zinazohusishwa na matumizi ya pombe.
Polisi na waendesha mashtaka wameagizwa kufungua upya kesi ambazo hazijatatuliwa zinazohusu wanawake na watoto, pamoja na kuharakisha kesi zinazoendelea, huku kipaumbele kikitolewa kwa kesi za ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake kwa sababu ya jinsia yao.






















