Hebu fikiria unakulia katika kambi ya wakimbizi, ukikimbia migogoro, lakini bado unakuwa na ndoto ya kuwa mwanariadha wa kimataifa.
Kwa wakimbiaji vijana wanne, ndoto hiyo sasa inawapeleka kwenye moja ya majukwaa makubwa zaidi ya michezo.
Leo tunakutana na wanariadha wakimbizi wanaoweka historia katika Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya mwaka 2026 jijini Dakar, Senegal; hii ni sehemu ya mfululizo wetu wa makala zinazoangazia vipaji vya riadha barani Afrika.
Wa kwanza ni Nyataba Gatloth, mwenye umri wa miaka 17, mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye aliwasili katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya mwaka 2022.
Anashiriki katika mbio za mita 800 na amekuwa akifanya mazoezi chini ya kocha Joseph Longok.
Ndoto yake ni kushinda medali na kuhamasisha vijana wengine wenye vipaji vya riadha kambini humo.
Kisha yupo Clement Niyomuhoza, mwenye asili ya Burundi, ambaye pia anaishi kambi ya Kakuma.
Mkimbiaji huyo wa mbio za mita 800 anasema kuchaguliwa kwake kumempa fursa ambayo hakuwahi kuifikiria.
Wanaoiwakilisha Uganda ni wakimbiaji wawili wa mbio fupi za mita 200.
Rachid Rochene, mwenye umri wa miaka 16, aliwasili nchini Uganda mwaka 2014 baada ya familia yake kukimbia mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kipaji chake kiligunduliwa wakati wa mazoezi, na ana ndoto ya kuweka rekodi mpya; anasema anahamasishwa na gwiji wa mbio fupi kutoka Jamaica, Usain Bolt.
Pia, Florence Masumbe, ambaye familia yake ilikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akiwa bado mtoto mchanga, anashiriki katika mbio za mita 200.
Anatarajia kukimbia umbali huo kwa sekunde 27 na kuonyesha uwezo walionao wanariadha wakimbizi.
Safari yao imejumuisha maandalizi makali katika Kituo cha Mafunzo ya Riadha cha ‘Complete Sports’ kilichopo Kaptagat, Kenya, katika eneo lenye mwinuko wa zaidi ya mita 2,400.
Pia wamepata muongozo na ushauri kutoka kwa Eliud Kipchoge, bingwa wa mbio za marathon katika Olimpiki mara mbili.
Kushiriki kwao ni tukio la kihistoria. Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Dakar 2026 ni mara ya kwanza kwa Timu ya Olimpiki ya Wakimbizi kushiriki katika mashindano hayo.
Na kuna mfano wa kuigwa unaoweza kuwapa hamasa.
Yiech Pur Biel, mwenye asili ya Sudan Kusini, alikulia katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma kabla ya kushiriki mbio za mita 800 katika Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, akiwa sehemu ya Timu ya Olimpiki ya Wakimbizi ya kwanza kabisa. Kwa sasa, yeye ni mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na mshauri kwa wanariadha vijana.
Ingawa huenda wakawa bado katika hatua za awali za taaluma zao za kimataifa, safari waliyoifanya yenyewe tayari ni mafanikio makubwa.
Kuanzia katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya na Uganda hadi kwenye ulingo wa kimataifa wa riadha, wanathibitisha kuwa kulazimika kuhama makazi hakumaanishi mwisho wa ndoto na matarajio yao.
Endelea kufuatilia TRT Afrika Swahili tunapoangazia vipaji vingine vipya na vya kusisimua katika ulimwengu wa riadha kutoka barani Afrika.


















