| Swahili
ULIMWENGU
3 dk kusoma
Trump: Marekani haihitaji msaada wa China wala Urusi ili kumaliza vita dhidi ya Iran
Akizungumza kabla ya mkutano wa pande tatu nchini China, Trump alidai kuwa jeshi la Marekani limeidhoofisha kwa kiwango kikubwa nguvu za kijeshi za Iran na kwamba Marekani inaudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz.
Trump: Marekani haihitaji msaada wa China wala Urusi ili kumaliza vita dhidi ya Iran
Trump amsema Urusi na China "zimetoa ushirikiano mzuri" na zimejizuia kupeleka meli za kivita katika eneo lenye mgogoro. / / Reuters

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa nchi yake haihitaji msaada wa China au Urusi katika juhudi za kumaliza vita dhidi ya Iran. Amesisitiza kuwa vikosi vya Marekani vimefanikiwa kuangamiza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kijeshi wa Iran.

"Hatuuhitaji msaada wowote. Tumelishinda jeshi lao la majini, tumelishinda jeshi lao la anga na tumeangamiza mifumo yao ya ulinzi wa anga," Trump aliliambia Shirika la Habari la Fox News mjini Shenzhen, China, siku ya Alhamisi.

Alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla ya kushiriki mkutano wa pande tatu pamoja na Rais wa China, Xi Jinping, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Trump pia alisema kuwa akiba ya makombora ya Iran imepungua na kufikia takribani asilimia 12 hadi 13 ya kiwango ilichokuwa nacho awali. Aliongeza kuwa Iran inataka kufikia makubaliano, hivyo Marekani haina sababu ya kuomba msaada kutoka kwa mataifa mengine. "Sitakwenda kuomba msaada wowote," alisema Trump.

Aidha, amesema kuwa jeshi la Marekani lina udhibiti kamili wa Mlango-Bahari wa Hormuz. Aliongeza kusema kuwa China na Urusi zimetoa ushirikiano mzuri kwa Marekani na hazijatuma meli zao za kivita katika eneo hilo lenye mvutano.

Makubaliano ya kudumu na Iran

Akizungumzia kuhusu kumaliza mzozo na Iran, Trump alisema viongozi wa Iran wanataka kufikia suluhu, lakini yeye analenga kupata makubaliano ya kudumu yatakayomaliza mgogoro huo.

"Nitamaliza jambo hili, na hivi karibuni, kwa njia moja au nyingine, tutalimaliza," alisema.

Alipoulizwa kwa nini atakutana na Xi Jinping na Vladimir Putin kwa wakati mmoja, Trump alisema kuwa viongozi hao wawili wanafanya kazi pamoja na wana uhusiano wa karibu.

Alidai kuwa Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ndiye aliyezisababisha China na Urusi kuwa karibu zaidi kutokana na masuala ya nishati.

"China inahitaji sana nishati, huku Urusi ikiwa na rasilimali nyingi za nishati," alisema Trump. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Marekani inaendelea kuwa na uhusiano mzuri katika uhusiano wake na mataifa hayo mawili na kuongeza kuwa viongozi wao wote wanampenda.

Trump atoa onyo kuhusu matumzi ya silaha za kemikali

Akizungumzia taarifa za kiintelijensia zinazodai kuwa Iran inaweza kuwa inafikiria kutumia silaha zisizo za kawaida dhidi ya Marekani, Trump alisema kuna viashiria vinavyoonyesha kuwa Iran inataka kutumia silaha za gesi na silaha za kibaiolojia.

"Kuna dalili kwamba Iran inataka kutumia silaha za gesi na za kibaiolojia, pamoja na mambo mengine. Hilo si jambo zuri. Ikiwa jambo hilo litatokea, tutawaangamiza kabisa," alisema.

Pia alikanusha madai kwamba baadhi ya wajumbe wa Baraza lake la Mawaziri wameamua kuishi ndani ya maeneo ya kijeshi kwa sababu ya vitisho vinavyotoka Iran.

Kauli za Trump zinakuja wakati ambapo mapigano makali yanaendelea kufuatia vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran Februari 28. Vita hivyo vilisababisha Iran kujibu kwa mashambulizi yaliyolenga maeneo mbalimbali nchini Israel na mataifa ya Ghuba yanayohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani.

Hati ya makubaliano ya maelewano iliyosainiwa mwezi Juni haikutekelezwa kikamilifu kutokana na kutokuelewana kuhusu masuala ya usalama wa usafiri wa baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Tangu mwezi Julai, mapigano ya hapa na pale yamekuwa yakijirudia, hali inayoendelea kuongeza mvutano katika eneo hilo.

CHANZO:TRT World and Agencies