Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kukatika kwa huduma ya umeme kwa muda katika mikoa 11 nchini, Novemba 14 na 15, 2026, kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni. Hatua hiyo inalenga kuwezesha kukamilishwa kwa kazi zinazohusiana na Mradi wa Usafirishaji Umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA).
Mikoa itakayoathirika na katizo hilo ni Singida, Manyara, Arusha, Kigoma, Kagera, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mwanza na Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Novemba 12, 2026, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji Umeme wa TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema katizo hilo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya mradi wa TAZA, ambao kwa sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji.
Ameeleza kuwa mradi huo unatarajiwa kuiwezesha Rukwa kuunganishwa na gridi ya Taifa ifikapo Disemba 5, 2026, hatua itakayoiwezesha mkoa huo kuacha kutegemea umeme kutoka Zambia.
Utekelezaji wa mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji na uhakika wa huduma ya umeme, sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi na kuvutia uwekezaji nchini.



















