Wasichana wa shule waliotekwa Nigeria wameachiwa huru
Wasichana 24 waliotekwa katika shule kaskazini-magharibi mwa Nigeria wiki iliyopita wameachiwa huru, msemaji wa gavana wa jimbo la Kebbi alisema siku ya Jumanne.
Wasichana hao walitekwa tarehe 17 Novemba wakati watu wenye silaha walivamia shule yao katika jimbo la Kebbi muda mfupi baada ya kikosi cha kijeshi kuondoka. Shambulio hilo limeongeza wimbi la utekaji katika majimbo ya Kwara na Niger, mamlaka zilisema.
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, siku ya Jumanne alipongeza kuachiwa kwa wasichana hao na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kuimarisha juhudi za kuwaokoa wengine ambao bado wanashikiliwa.
“Nimepata faraja kwamba wasichana wote 24 wamepatikana. Sasa ni lazima, kama jambo la dharura, kuongeza idadi ya askari katika maeneo yaliyo hatarini ili kuzuia matukio zaidi ya utekaji. Serikali yangu itatoa msaada wote unaohitajika kufanikisha hili,” Tinubu alisema.
Utekaji wa watu kwa ajili ya kupata fidia imekuwa jambo la kawaida kaskazini mwa Nigeria, ambako magenge yenye silaha hulenga shule na jamii za vijijini, mara nyingi wakizidi nguvu vikosi vya usalama vya eneo.