Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye amesema kuwa Serikali inapaswa kuangalia upya suala la kufungwa kwa Ziwa Tanganyika kwa kuwa wananchi wengi wa Kigoma wanategemea Ziwa hilo kujipatia kipato na chakula.
Alipochangia bungeni, Katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mayeye amesema kuwa kupungua na kuongezeka kwa samaki ni jambo la kawaida katika ziwa hilo kwani kuna nyakati Ziwa “linajifunga na kujifungua” na samaki kuongezeka wenyewe.
Amesema kipindi cha kufungwa kwa Ziwa wananchi wengi hukosa samaki na hata hulazimika kula samaki wanaotoka Mwanza, huku akieleza kuwa maisha ya watu wengi wa Kigoma yanategemea uvuvi kwa ajili ya kusomesha watoto na kuhudumia familia zao.
Pia amesema kipindi cha kufungwa kwa Ziwa ndicho ambacho vitendo vya uvuvi haramu na wizi huongezeka, akidai kuwa nyavu haramu nyingi zinaingia kutoka nje ya nchi huku zikilipiwa kodi lakini baadaye kuambiwa ni haramu kwa wavuvi.
Mbunge huyo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa wavuvi kukata leseni za mwaka badala ya kulipia mara kwa mara kutokana na hali ngumu ya kifedha waliyonayo.
Aidha, ameieleza Serikali kuongeza ulinzi kwa wavuvi wa Ziwa Tanganyika kutokana na matukio ya uporaji na kushambuliwa yanayoripotiwa Ziwani humo.
Kauli ya Mayeye imekuja wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa na kupitishwa bungeni Mei 14, ambapo Serikali ilieleza mpango wa kufunga baadhi ya maziwa kwa kipindi cha miezi mitatu, ikiwemo Ziwa Tanganyika, kwa lengo la kuhifadhi mazalia ya samaki na kuongeza uzalishaji wa rasilimali hiyo muhimu.
Hata hivyo, utaratibu wa kufunga maziwa si jambo jipya nchini Tanzania, kwani umekuwa ukifanyika kila mwaka kama sehemu ya juhudi za Serikali za kulinda samaki dhidi ya uvuvi uliopitiliza na kutoa nafasi kwa mazalia kuongezeka.
















