Bodi ya Amani ya Trump na maana yake kwa mustakabali wa Palestina

Mpango wa amani uliozinduliwa Davos unauweka ulimwengu mbele ya fursa ya kipekee: kuwapa Wapalestina haki yao ya kuishi kwa heshima na uhuru — au kuhatarisha kuugeuza kuwa jaribio jingine lililofeli.

By
Tathmini yoyote ya kweli ya Bodi ya Amani lazima ianze na rekodi yake ya kisiasa. / / Reuters

Mara nyingi, mipango ya kimataifa kuhusu Palestina inapozinduliwa katika majukwaa kama Davos, huwasilishwa kwa lugha inayoashiria kuwa haina budi kutokea. Amani huonekana kama tatizo la kiufundi linaloweza kutatuliwa kupitia vikao, mifumo na makubaliano yanayosimamiwa kwa uangalifu.

“Bodi ya Amani” iliyozinduliwa katika Jukwaa la Uchumi Duniani ni jaribio jipya la kuleta msukumo katika mgogoro uliodumu kwa vizazi vingi.                                                                            

Kwa Wapalestina, matukio kama haya si mapya. Ni sura zinazojirudia katika historia ndefu ya “suluhisho” zilizobuniwa kutoka nje — nyingi zikiwa na ahadi za dola, utulivu au ustawi, lakini matokeo yake yakiwa ni kuendelea kwa ukaliaji wa mabavu, mamlaka yaliyogawanyika, na kuungwa mkono dhuluma badala ya suluhu.

Kwa hiyo, tathmini yoyote makini ya Bodi ya Amani lazima ianze si tu kwa matarajio yake, bali kwa rekodi ya kisiasa inayoirithi.

Rais wa Marekani Donald Trump alizindua Bodi ya Amani kama chombo cha kutatua migogoro ya kimataifa, kwa gharama inayoripotiwa kufikia dola bilioni moja kwa wanachama wa kudumu.

Awali, bodi hiyo ilikusudiwa kusimamia ujenzi upya wa Gaza, lakini rasimu ya katiba yake haionyeshi kuweka mipaka ya jukumu lake katika ardhi ya Palestina pekee.

Afisa mmoja mwandamizi wa Ikulu ya White House amesema kuwa takribani nchi 35 — ikiwemo Uturuki — zimekubali kujiunga hadi sasa, kati ya mialiko karibu 50 iliyotumwa.

Maelezo haya ni muhimu. Yanaweka wazi kuwa Bodi ya Amani si chombo cha kibinadamu tu kinacholenga Gaza pekee, bali ni muundo mpya wa kisiasa wenye matarajio mapana, na uanachama wake unaoamuliwa na nguvu, na uwiano wa kisiasa.

Amani kwa namna gani?

Michakato ya amani haiegemei upande wowote. Huakisi mizani ya nguvu na vipaumbele vya kisiasa vilivyopo wakati wa kuanzishwa kwake, na mchakato huu hauna tofauti.

Muundo wa bodi unaongeza wasiwasi huu. Miongoni mwa nchi zinazodaiwa kushiriki ni Israel na baadhi ya washirika wakuu wa Marekani ambao ni Mashariki ya Kati, pamoja na serikali nyingine zilizo na uhusiano wa karibu wa kisiasa na Washington.

Ushiriki wa Israel ni wenye uzito mkubwa. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu — ambaye serikali yake ilisimamia uharibifu mkubwa wa Gaza — yupo kama sehemu ya bodi inayodaiwa kuunda amani na ujenzi upya.

Hili halifanyi mpango huo kuwa batili moja kwa moja, lakini linaonyesha mvutano wa msingi uliokumba juhudi nyingi za kidiplomasia kuhusu Palestina: je, amani inachukuliwa kama mchakato unaojengwa juu ya uwajibikaji na haki, au kama jukwaa la kudumisha nguvu bila ya kuwepo kwa uwajibikaji?

Mvutano huu unaeleza kwa nini mashaka ya Wapalestina kuhusu mifumo mipya ya kidiplomasia si msimamo wa kiitikadi tu, bali ni uzoefu halisi wa kisiasa.

Kuanzia Oslo na kuendelea, mipango ya amani mara nyingi imeipa kipaumbele uratibu wa usalama, usimamizi wa uchumi na makubaliano ya mpito, huku ikiahirisha au kupunguza masuala ya msingi ya mgogoro: ukaliaji wa mabavu, mamlaka kamili, mipaka, wakimbizi na usawa mbele ya sheria.

Matokeo hayakuwa amani, bali kuongezeka kwa nguvu iliyoimarisha ukaliaji wa Israel na kudhoofisha matumaini ya dola huru ya Palestina.

Hatari ya Bodi ya Amani si tu kwamba inaweza kufeli. Hatari kubwa ni kwamba inaweza “kufanikiwa” kwa kuubadili mgogoro kwa namna inayopunguza matarajio.

Ujenzi upya bila mamlaka, misaada bila haki, na utulivu bila haki ya kijamii ni matokeo yaliyozoeleka ya michakato ya zamani.

Bodi itakayochukulia Gaza kama changamoto ya kiufundi ya ujenzi pekee, badala ya kuwa sehemu ya mapambano mapana ya kisiasa ya kujitawala, iko katika hatari ya kurudia makosa hayo.

Maono ya Trump ya Gaza iliyojengwa upya, yenye majengo ya kifahari na fukwe zilizojaa mitende, ni dhihaka kwa mateso waliyopitia Wapalestina wa Gaza katika miaka miwili iliyopita, ardhi yao ya nyumbani ikigeuzwa kuwa mandhari ya kutisha na mashine ya vita ya Israel.

Hata hivyo, itakuwa si sahihi — na si busara kimkakati — kuipuuza Bodi ya Amani kama jambo lisilo na maana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, aliweka suala hili katika muktadha sahihi alipoiita Bodi ya Amani “fursa ya kihistoria” ya kumaliza mateso ya muda mrefu ya Wapalestina.

Mtazamo wake unaakisi matumaini ya Rais Recep Tayyip Erdogan — mmoja wa watetezi wakubwa wa suala la Palestina — kwamba mipango yote inayolenga kuleta amani Gaza ni ya muhimu.

Mipango ya ukubwa huu huunda mjadala wa kidiplomasia, huathiri matarajio ya kimataifa, na huweka viashiria ambavyo vinaweza kuendeleza au kudhoofisha madai ya Wapalestina.

Wapalestina wakikubali au la, chombo kama hiki kitaathiri namna serikali, vyombo vya habari na taasisi zinavyozungumzia “suluhisho” katika miezi ijayo. 

Kwa maana hiyo tu, Bodi ya Amani inaweza kuitwa fursa ya kipekee, licha ya mapungufu yake ya kimsingi.

Si kwa sababu muundo wake unahakikisha haki, bali kwa sababu nyakati za umakini mkubwa wa kimataifa hulazimisha maamuzi ambayo kwa kawaida huahirishwa.

Huzilazimisha nchi na taasisi kueleza wazi kile ambacho wako tayari kukitetea, na kile ambacho wako tayari kukiachia.

Ni ufaulu sasa au kutofaulu tena

Ili fursa hii iwe na maana, kanuni fulani haziwezi kubaki katika kiwango cha matarajio au maneno tu. Sheria ya kimataifa lazima ichukuliwe kama mfumo unaofunga kisheria, si mrejesho wa kisiasa tu.

Haki ya Wapalestina ya kujitawala haiwezi kunedelea kuahirishwa kwa kisingizio cha motisha za kiuchumi au mipango ya usalama.

Ukaliaji wa mabavu lazima utajwe wazi kama kikwazo kikuu cha kupatikana kwa amani, si kufichwa nyuma ya lugha ya “mizunguko ya vurugu” au “kutokuaminiana”.

Muhimu zaidi, ushiriki wa Wapalestina lazima uwe wa maana, si wa ishara tu. Mipango mingi ya awali iliwajumuisha Wapalestina kwa sura ya nje huku ikipuuzia madai yao ya kisiasa.

Mchakato unaotafuta uhalali bila usawa hauwezi kuleta utulivu, kando na kuleta maridhiano.

Jukumu la jumuiya pana ya kimataifa — hasa ulimwengu wa Kiislamu — ni la msingi. Ushiriki katika bodi kama hii haupaswi kupuuzwa.

Ikiwa nchi zitaamua kushiriki, lazima ziweke mipaka iliyo wazi: dola ya Palestina haiwezi kuwa hiari; ratiba haziwezi kunyooshwa bila kikomo; ujenzi upya hauwezi kutenganishwa na haki za kisiasa.

Ushiriki bila nguvu ya kushinikiza una hatari ya kuhalalisha matokeo yanayosimamia mgogoro badala ya kuyatatua.

Pia kuna hatari pana kwamba mipango kama Bodi ya Amani itakuwa chombo cha kuhalalisha mahusiano ya kawaida bila suluhisho la kweli.

Ushirikiano wa kikanda na ujumuishaji wa kidiplomasia unaweza kusonga mbele, huku suala la Palestina likibaki bila kutatuliwa kimuundo.

Njia hii imejaribiwa hapo awali, na matokeo yake yanaonekana: vurugu zinazorudiwa, ukosefu wa usawa unaozidi, na kuporomoka kwa imani katika suluhisho za kisiasa.

Amani haitokani na vikao pekee. Haitokani na makubaliano ya watu wenye hadh ya juu au miundo ya taasisi ikiwa hayaunganishwi na haki halisi mashinani.

Amani hutokea pale ambapo nguvu zinadhibitiwa na sheria, haki zinachukuliwa kuwa msingi usioweza kujadiliwa, na wale wanaoathirika zaidi hawalazimishwi kubadilisha mustakabali wao kwa utulivu wa muda mfupi.

Kwa hiyo, Bodi ya Amani itahukumiwa si kwa umaarufu wa wadhamini wake au ukubwa wa malengo yake, bali kwa kipimo rahisi: je, inakabiliana na uhalisia wa ukaliaji wa mabavu na ukosefu wa usawa, au inajaribu kuvisimamia tu?

Ikiweza kufanya hivyo, basi huenda kweli ikawa fursa adimu ya kuvunja mienendo ya miong kadhaa za mbinu zilizoshindwa.

Uamuzi hauko mikononi mwa Wapalestina pekee. Uko pia mikononi mwa jumuiya ya kimataifa ambayo inaendelea kuunda — na mara nyingi kulinda — mazingira yanayoufanya mgogoro huu uendelee kuwepo.