Ufalme wa kijadi wa Uganda umemteua mtangazaji wa televisheni siku ya Jumatano kumrithi Mfalme Oyo Nyimba, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 34 baada ya kuwa mfalme mwenye umri mdogo zaidi duniani aliposhika hatamu akiwa na miaka 3.
Oyo Nyimba alifariki dunia Agosti 27 nchini Marekani ambapo alikuwa anatibiwa maradhi ya saratani.
Pamoja na Uganda kuwa jamhuri, Oyo Nyimba amekuwa kiongozi wa Tooro magharibi mwa Uganda, moja ya falme za koloni hilo la zamani la Uingereza, ambao unakuwa na ushawishi mkubwa wa kitamaduni na kijamii.
Katika mkutano na waandishi wa habari kutoka makao makuu ya ufalme mjini Fort Portal, Kamati ya ukoo wa kifalme kuhusu mrithi ilimtangaza Mwanamfalme Edward Rukidi Kijanangoma, mtangazaji na mhariri wa shirika la habari la serikali UBC, kuwa mfalme.
Oyo Nyimba, balozi wa hisani wa Umoja wa Mataifa alikuwa mfalme mwenye umri mdogo zaidi mwaka 1995 akiwa na miaka 3.
Kuteuliwa kwa Kijanangoma kumehitalifiana na tangazo la awali la Waziri Mkuu wa ufalme huo Calvin Armstrong Rwomiire, ambaye alisema kuwa mfalme Oyo Nyimba aliyekuwa hajaoa, aliacha mtoto atakayemrithi katika nafasi hiyo.
Mwili wa Oyo Nyimba umerudishwa Uganda kutoka Marekani siku ya Ijumaa na atazikwa siku ya Jumamosi kwenye makaburi ya kifalme karibu na kasri lake mjini Fort Portal.





















