Wanaoshukiwa kuwa magaidi wa Boko Haram wamewaua wanajeshi wasiopungua 10 na kujeruhi wengine 20 katika mashambulizi kwenye kambi ya jeshi jimbo la kaskazini mashariki la Nigeria la Borno wiki hii, vyanzo vya kijeshi na wananchi vilisema siku ya Alhamisi.
Magaidi hao walishambulia kambi ya jeshi ilioko eneo la Guzamala usiku wa Jumanne na kuchoma moto nyumba katika kijiji cha karibu cha Mairari, vyanzo viwili vya kijeshi vilisema.
Zaidi ya watu 20 walijeruhiwa katika shambulio hilo, huku raia wasiopungua watano na mlinzi wa misitu wakiuawa, vyanzo hivyo vilisema kwa sharti ya kutotajwa kwa sababu hawajaidhinishwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Msemaji wa jeshi Kapteni Mohammed Goni hakujibu alipotakiwa kuzungumzia shambulio hilo.
Wachukua madau ya uvuvi
Kabla ya shambulio hilo kwenye kambi ya jeshi, magaidi hao walichukua madau 40 ya uvuvi eneo la Tumbun Barebari, kijiji cha karibu , amesema Jibrin Hassan, mvuvi ambaye dau lake lilichukuliwa.
Babagana Muhammad, mvuvi mwingine, amesema "ilikuwa mashambulio ya wakati mmoja ... tofauti ni kuwa sisi wavuvi hatukudhuriwa".
Oparesheni ya jeshi la Nigeria imekuwa ikikabiliana na changamoto za ukosefu wa usalama kwa miongo miwili kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Wiki iliopita, vikosi vya Nigeria vilikabiliana na wapiganaji hao katika jimbo la Borno, na kuwaua magaidi zaidi ya 25.




















