Erdogan na Mwanamfalme wa Saudia waunga mkono umoja wa Somalia, wajadili masuala ya kikanda
Viongozi wa Uturuki na Saudi Arabia wamepinga vikali harakati za kujitenga na mifumo sambamba katika Pembe ya Afrika walipokutana jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Uturuki na Saudi Arabia zimethibitisha tena kuunga mkono mamlaka kamili na uhuru wa mipaka ya Somalia, na kukataa kile walichokiita hatua za kujitenga na mifumo sambamba inayotishia umoja wa taifa hilo la Pembe ya Afrika. Haya yaliangaziwa wakati Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alipokutana na Mwanamfalme Mohammed bin Salman mjini Riyadh katika ziara yake rasmi ya siku moja.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki iliyotolewa Jumatano, viongozi hao wawili katika mkutano wao uliofanyika siku ya Jumanne jijini Riyadh walisisitiza “uungaji mkono thabiti” kwa umoja wa nchi ya Somalia na kwa kuimarisha utulivu, maendeleo na ustawi wa wananchi wake.
Pia walilaani hatu ya Israel kuitambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru na vilevile Somaliland kuitambua Israel kama taifa huru, wakisema kuwa hatua hiyo inaendeleza vitendo vya upande mmoja vya kujitenga, inakiuka sheria za kimataifa na inaongeza mvutano wa kikanda.
Mwishoni mwa Disemba mwaka jana, Israel ilitangaza kuwa imeitambua Somaliland kama taifa huru.
Somaliland imekuwa ikijiendesha kama eneo lenye mamlaka ilipotangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991. Hata hivyo, haijapata kutambuliwa rasmi kimataifa, huku serikali ya shirikisho ya Somalia ikisisitiza mara kwa mara kuwa eneo hilo ni sehemu isiyotenganishwa ya ardhi yake.
Msaada wa pamoja kwa serikali halali ya Yemen
Kuhusu suala la Yemen, Uturuki na Riyadh zilisisitiza kuunga mkono kwao serikali halali ya nchi hiyo, inayowakilishwa na Baraza la Uongozi wa Rais na serikali ya Yemen. Pia walisisitiza umuhimu wa kulinda mamlaka, umoja na uhuru wa mipaka wa Yemen.
Upande wa Uturuki uliunga mkono nafasi ya Saudi Arabia nchini Yemen pamoja na juhudi zinazoongozwa na mkuu wa Baraza la Uongozi wa Rais katika kutatua mgogoro na kufanikisha maridhiano ya kitaifa, ikiwemo wito wa kuitishwa kwa mkutano jumuishi jijini Riyadh utakaowaleta pamoja makundi yote ya eneo la kusini mwa Yemen.
Kulinda umoja wa Sudan
Kuhusu Sudan, nchi hizo mbili zilithibitisha msimamo wao thabiti wa kulinda umoja, usalama na uhuru wa Sudan, huku zikikataa mifumo sanjari na mifumo yoyote isiyo halali iliyo nje ya taasisi halali za nchi.
Walisisitiza haja ya kuzuia Sudan kuwa kitovu cha migogoro, shughuli haramu na uingizaji wa silaha za kigeni kinyume cha sheria, huku wakihimiza ulinzi wa raia na uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu na Azimio la Jeddah la Mei 2023.
Uturuki ilipongeza juhudi za Saudi Arabia za kusaidia kumaliza vita na kupunguza mateso ya wananchi wa Sudan, huku Riyadh ikitoa shukrani kwa Uturuki kwa msaada wake wa kibinadamu na juhudi za kukabiliana na majanga.
Pande zote mbili zilipongeza uamuzi wa Jeshi la Sudan wa kuendelea kufungua mpaka wa Adre na Chad kwa muda mrefu zaidi, pamoja na kufungua tena viwanja kadhaa vya ndege na mipaka ili kurahisisha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu.
Erdogan na Mwanamfalme wa Saudi wataka Israel iondoke Syria
Kuhusu Syria, Uturuki na Saudi Arabia zilisifu kile walichokiita hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa na serikali ya Syria katika kulinda usalama, uthabiti na uhuru wa mipaka ya nchi hiyo, na zikakaribisha juhudi za kimataifa za kuisaidia Syria na kuondoa vikwazo.
Waliunga mkono makubaliano ya kusitisha mapigano na ya kujumuisha yaliyoanzishwa Januari 30, wakathibitisha kuunga mkono juhudi za kupambana na makundi ya kigaidi na kukuza amani ya kiraia, na wakalaani ukiukwaji wa mara kwa mara wa uhuru wa Syria unaofanywa na Israel.
Pande hizo mbili zilisisitiza wito wao kwa Israel kujiondoa mara moja katika maeneo yote ya Syria inayoyakalia, zikitahadharisha kuwa mashambulizi yanayoendelea yanadhoofisha sheria za kimataifa na kuhatarisha kusambaa kwa mgogoro mpana wa kikanda.