| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Marekani imemwekea vikwazo Kabila kwa madia ya kuunga mkono waasi Mashariki mwa Congo
Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila anatuhumiwa kuunga mkono waasi mashariki mwa nchi hiyo na kuwahimiza wanajeshi wa Congo kujitenga na jeshi lao.
Marekani imemwekea vikwazo Kabila kwa madia ya kuunga mkono waasi Mashariki mwa Congo
Joseph Kabila alikuwa rais wa DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019./ / Reuters

Nchi ya Marekani siku ya Alhamisi ilitangaza kuweka vikwazo dhidi ya rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila, kwa madai ya kuunga mkono waasi wa AFC/M23.

Idara ya Hazina ya Marekani, kupitia Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC), katika taarifa yake ilimtuhumu Joseph Kabila kwa kutoa msaada wa kifedha kwa AFC ili kuathiri hali ya kisiasa mashariki mwa Congo, na pia kuwahimiza wanajeshi wa nchi hiyo kujitenga na kujiunga na safu za waasi.

Hatua hizo za vikwazo zinajumuisha hasa kufungiwa kwa mali za Kabila nchini Marekani, pamoja na marufuku rasmi kwa raia au taasisi yoyote ya Marekani kufanya biashara naye.

“Rais Donald Trump anaweka msingi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na ameweka wazi kwamba wale wanaoendelea kusababisha machafuko watawajibishwa,” alisema Waziri wa Hazina Scott Bessent.

Kundi la M23 limekuwa kitovu cha mzozo mashariki mwa Congo. Kundi hilo la waasi, linalodaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda kulingana na Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi, linadhibiti maeneo makubwa mashariki mwa nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu, ambayo ilitekwa mapema mwaka 2025.

Congo na Rwanda zilitia saini makubaliano ya kihistoria ya amani mjini Washington DC tarehe 4 Disemba, yakilenga kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa katika sehemu ya mashariki ya nchi hiyo.

Hata hivyo, mapigano yaliendelea wiki hii, na kusababisha tena watu wengi kuhama makazi yao, kulingana na vyanzo vya ndani.

Bessent alisema: “Idara ya Hazina itaendelea kutumia zana zake zote kuunga mkono utekelazaji wa Makubaliano ya Washington.”

Kabila alichukua madaraka nchi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019. Tangu mwaka 2023, amekuwa akiishi Afrika Kusini.

Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka 2025, alionekana hadharani mashariki mwa Congo na kuonyesha nia ya kurejea nyumbani “kuchangia kutafuta suluhisho” la mgogoro unaoendelea.

Mahakama ya kijeshi ya Congo mwaka jana ilimhukumu Kabila kwa hukumu ya kifo akiwa hayupo nchini, kwa mashtaka ya uhaini na uhalifu wa kivita.

CHANZO:AA