Zijue alama na vivutio maarufu Afrika Mashariki
Mnara wa Askari, maarufu kama 'Mnara wa Bismini' uliopo katikati ya jiji la Dar es Salaam./Picha:Wengine
Zijue alama na vivutio maarufu Afrika Mashariki
Afrika Mashariki ni eneo lilijipambanua kwa alama na vivutio mbalimbali vyenye kuwakilisha utambulisho wa eneo hilo.

Miji mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki hujulikana zaidi kwa baadhi ya alama au vivutio ambavyo husadifu utambulisho wake.

Kwa mfano, jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, liliwahi kujipatia umaarufu mkubwa kupitia sanamu la Askari, maarufu kama Bismini, linalopatikana maeneo ya Posta.

Ilikuwa ni kawaida kusikia watu wakisema, huwezi kudai umefika Dar es Salaam, kama hujamwona huyo askari au hata kupiga naye picha.

Kisha, zikaja alama nyingine kama vile majengo pacha ya BOT, daraja la Selander, daraja la Tanzanite, daraja la Nyerere kule kigamboni.

Ukienda kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, yaani Dodoma, basi utakutana na mnara wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, uliopo katika bustani la Nyerere Square iliyopo katikati ya jiji hilo.

Pale Arusha, upo mnara wa azimio, ambao ulijengwa kama kumbukumbu ya kuadhimisha miaka 10, tangu Tanzania ijipatie uhuru.

Jijini Nairobi nchini Kenya, jengo la Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano la Jomo Kenyatta, maarufu kama KICC.

Likiwa lina urefu wa futi 344, jengo hilo lilizinduliwa mwaka 1973.

Ukisogea pale mji wa pwani wa Mombasa, utakutana na pembe mbili za ndovu, ambazo ni kiashirio kuwa sasa umeingia Mombasani.

Ukienda jijini Kampala, utakutana na kasri la mtawala wa Baganda, anayejulikana kama Kabaka.

Kasri hili ambalo linapatikana katika eneo la Lubiri ambalo lipo katika moja ya miinuko saba ya jijini Kampala.

Kifupi ni kwamba, usimamapo sehemu yoyote jijini Kampala, basi utayaona makazi haya.

Pia upo msikiti wa Gaddafi, maarufu kama msikiti wa taifa jijini Kampala.

Jijini Bujumbura, kuna mnara unaofahamika kama Monument de l'Unite au mnara wa Umoja.

Kivutio hiki kilizinduliwa mwaka 2002, kuwaenzi watu waliopoteza maisha wakati wa machafuko nchini humo.

Pale nchini Rwanda, lipo eneo maalumu la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, lililopo Gisozi jijini Kigali.

Eneo hili limekuwa kama kivutio cha utalii, na watu wengi hutembelea hapa kuja kupata historia ya mauaji hayo.

Pia upo ukumbi wa Kimataifa wa Kigali, maarufu kama KCC.

Jijini Kinshasa, ipo makumbusho ya Patrice Lumumba, waziri mkuu wa kwanza wa DRC.

Eneo hili huvutia watu wengi kila mwaka.

Hapo hapo Kinshasa, ipo pia makumbusho maalumu ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent-Désiré Kabila.

CHANZO:TRT Afrika Swahili