Mfanyakazi wa shirika la misaada aliyetaka Joseph Kony kukamatwa aachiwa huru nchini CAR
Joseph Martin Figueira alikuwa anahudumu kifungo cha miaka 10 jela akishtumiwa kutaka usaidizi wa kundi lenye silaha kumkamata kiongozi wa waasi wa Uganda Joseph Kony
Jamhuri ya Afrika ya Kati imeamuachilia huru mfanyakazi wa shirika la misaada la Marekani anayeshtumiwa kutaka kundi lenye silaha kumkamata kiongozi wa waasi wa Uganda Joseph Kony, Ureno imesema.
Joseph Martin Figueira, raia wa Ubelgiji na Ureno anayefanya kazi na shirika la Family Health International 360, alikuwa anatarajiwa kuwasili mjini Lisbon kwa ndege ya kijeshi siku ya Jumanne, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ureno aliiambia AFP.
Baada ya kukamatwa kwake Mei 2024, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na kazi ngumu mwezi Novemba kwa kutatiza usalama wa nchi katika taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Alishtakiwa kwa kupanga njama na ujasusi kwa kuwasiliana na wapiganaji katika eneo lenye ukosefu wa usalama la mashariki la Haut-Mbomou, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.
Mwendesha mashtaka wa umma alimshtumu kwa "kutoa amri" kwa kundi la wapiganaji lenye ushawishi kumsaka Kony, kiongozi muasi wa kundi la Lord's Resistance Army ambaye anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Huku Kony akifahamika kuendeleza harakati zake katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, hajawahi kuonekana hadharani tangu 2006.
Kulingana waziri wa mambo ya nje wa Ureno, kuachiliwa huru kwa Figueira ni kutokana na juhudi za kidiplomasia za muda mrefu zilizohusisha serikali zote za Ureno na Ubelgiji, pamoja na Umoja wa Ulaya.