| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Somalia yaripoti kumuua mshirika wa kiongozi wa Al Shabab, Ahmed Diriye
Serikali ya Somalia imeripoti kumuua kiongozi wa kigaidi aliyekuwa mshirika wa karibu wa kiongozi wa Al Shabab, Ahmed Diriye.
Somalia yaripoti kumuua mshirika wa kiongozi wa Al Shabab, Ahmed Diriye
Jeshi la Somali limeimarisha mapambano yako dhidi ya kundi la Alshabaab. / / AA
tokea masaa 8

Kiongozi huyo wa kigaidi, Mohamed Sahal Idle, alilengwa na kuuawa katika operesheni ya kiusalama iliyofanyika katika eneo la kati la Juba linalodhibitiwa na kundi Al Shabab, kulingana na taarifa ya mamlaka.

Shirika la Taifa la Ujasusi na Usalama la Somalia (NISA) lilitangaza Jumanne kwamba limemuua kiongozi mwandamizi wa Al Shabab katika operesheni ya kiusalama.

NISA ilisema kuwa Mohamed Sahal Idle, anayejulikana pia kwa jina la utani Abu Usaama, aliuawa katika operesheni iliyofanyika kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa karibu na mji wa Sakow, katika eneo la Middle Juba linaloshikiliwa na Al Shabab.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Usaama alikuwa maarufu kwa uhalifu wake dhidi ya wananchi wa Somalia na alikuwa mshirika wa karibu wa kiongozi wa kundi hilo, Ahmed Diriye.

NISA ilieleza kuwa alikuwa akiandaliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa fedha wa Al Shabab, Abdullahi Wadaad, ambaye aliuawa katika operesheni iliyoongozwa na NISA huko Kuunyo Barrow, eneo la Lower Shabelle, mwezi Januari mwaka huu.

“Abu Usaama alikuwa na jukumu la kuwatoza wananchi wa Somalia pesa kwa nguvu na kupora mali zao,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Al Shabab ilithibitisha katika taarifa kwamba Mohamed Abu Usaama, aliyekuwa mkuu wa kamati ya kundi hilo inayoshughulikia masuala ya ukame, aliuawa katika shambulio la anga lililofanyika pembezoni mwa mji wa Sakow.

Kundi hilo la kigaidi lenye uhusiano na Al Qaeda limekuwa likifanya mashambulizi nchini Somalia kwa zaidi ya miaka 16, likilenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali na raia.

Tangu Julai mwaka jana, jeshi la Somalia, kwa msaada wa Misheni ya Umoja wa Afrika ya Kusaidia na Kustawisha Utulivu nchini Somalia (AUSSOM) pamoja na washirika wengine wa kimataifa, limeongeza operesheni dhidi ya Al Shabab.

Mamlaka ya misheni hiyo ya Umoja wa Afrika iliongezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Disemba kwa mwaka mwingine, kupitia azimio lililoongeza ruhusa ya operesheni hiyo hadi Desemba 31.

CHANZO:AA