Kenya yalipa ada ya Dola milioni 30 ya uenyeji wa AFCON 2027

Wiki moja iliyopita, Kenya ilipewa siku 10 pekee, iwe imelipa kiasi hicho, kama sehemu ya ada ya kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2027, au kukosa haki ya kuwa mwenyeji mwenza pamoja na majirani zake Uganda na Tanzania.

By
Rais William Ruto wa Kenya akiwa na rais wa FIFA Giovanni Infantino na yule wa CAF, Patrice Motsepe./Picha:Wengine

Baada ya wiki kadhaa za sintofahamu, hatimaye serikali ya Kenya imelipa ada ya kiasi cha Dola milioni 30 (bilioni 3.9 za Kenya), kama ada ya kuandaa michuano ya AFCON 2027, hapo mwakani.

Katika taarifa yake iliyotolewa Machi 31, 2026, waziri wa michezo wa nchi hiyo, Salim Mvurya amesema kuwa Kenya imefanikiwa kulipa ada hiyo, kama ilivyokuwa imeelekezwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

“Kenya imekidhi moja ya vigezo vya kuandaa mashindano ya AFCON kwa kulipa ada hiyo kwa CAF,” alisema Mvurya.

Wiki moja iliyopita, Kenya ilipewa siku 10 pekee, iwe imelipa kiasi hicho, kama sehemu ya ada ya kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2027, au kukosa haki ya kuwa mwenyeji mwenza pamoja na majirani zake Uganda na Tanzania.

Katibu wa Wizara ya Michezo, Elijah Mwangi, aliwajulisha Wabunge wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Michezo kuwa barua kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeweka tarehe ya mwisho ya Machi 30 kwa Kenya kukamilisha malipo hayo.

Kulingana na Mwangi, Tanzania na Uganda zilikuwa zimekamilisha malipo yao.

Michuano ya AFCON 2027, inaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.