| Swahili
Maoni
AFRIKA
5 dk kusoma
Hifadhi ya Jamii Barani Afrika: Nguvu ya Ubuntu
Bara la Afrika bado lipo nyuma katika utekelezaji wa sera za hifadhi ya jamii, ukilinganisha na maeneo mengine ulimwenguni, hali inayowaacha wananchi wake katika mazingira hatarishi.
Hifadhi ya Jamii Barani Afrika: Nguvu ya Ubuntu
Mifuko ya kijamii ina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii za kiafrika./Picha:UNDP
19 Januari 2026

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, hali ya hifadhi ya jamii barani Afrika inayotambulika kama “mkusanyiko wa sera na mipango inayolenga kuzuia au kuwalinda watu wote dhidi ya umaskini, udhaifu na kutengwa kijamii katika hatua zote za kimaisha” — umeendelea kukua maradufu.

Kulingana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, sekta hii imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya watu, hasa kupitia mifuko yake mbalimbali, kama vile mifuko ya afya, uhaliwishaji fedha, ujenzi na mengineyo. Ukuaji huu unaelekezwa katika kupunguza umaskini kwa makundi yaliyo hatarini yakiwemo kama vile watoto, wanawake na watu wenye ulemavu (UNDP, 2019).

Licha ya jitihada hizi,  changamoto mbalimbali zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa rasilimali za kifedha, hali ya kisiasa isiyo imara na udhaifu wa taasisi, bado zinaendelea kuhatarisha maendeleo na hivyo kudhoofisha ufanisi wa sera na programu za hifadhi ya jamii.

Hadi leo, bara la Afrika bado lipo nyuma katika utekelezaji wa sera ya hifadhi ya jamii, ukilinganisha na maeneo mengine ulimwenguni, hali inayowaacha wananchi wake katika changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Hii ni kulingana na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Makala hii inalenga kuonesha umuhimu wa vikundi vya kijumuia vya hifadhi ya jamii barani Afrika.

Kuanzia ngazi za chini

Vikundi vya kijumuia vya hifadhi ya jamii – kuanzia hapa huitwa vikundi- vinafaamika kama community-based social protection organisations kwenye lugha ya Kiingereza.  Vikundi hivi ni taasisi au mipango iliyo na misingi wa kijamii; inayoundwa na mitandao isiyo rasmi kwa ajili ya kutoa misaada ya kiuchumi kwa watu mbalimbali. Mifano ya vikundi hivi ni vikoba, chama, susu nk.

Kwa kawaida vikundi hivi  huundwa na wanachama kuanzia 10 hadi 40, na kwa muda mrefu, vimekuwa nguzo muhimu ya maisha kwa jamii hususani kwenye jamii ambazo mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii imeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Vikundi hivi vimelinganishwa na kuonekana kushabihiana na sera zinazoendeshwa na taifa, hasa katika majukumu yao; licha ya kutofautiana katika wigo wa huduma, aina ya huduma, mifumo ya uongozi na uwajibikaji.

Mwishoni mwa mwaka 2025, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kwa pamoja, walizindua ripoti iliyochunguza vikundi katika mataifa matano, ikiwemo vijiji 24 na kaya 2,400.

Matokeo ya utafiti huu yanatoa taswira madhubuti inayoonyesha mustakabali wa vikundi hivi barani Afrika.

Vikundi hivi vinanufaishaje jamii?

Manufaa

Wanachama wa vikundi hivi hupokea misaada mbalimbali ikiwemo  uwezeshaji wa kifedha na wakati mwingine wa kihisia, pamoja na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kitamaduni.

Hali kadhalika, vimekuwa na msaada mkubwa kwa vijana, hasa wanapokuwa wakuu wa kaya au wanapojiandaa na ndoa.

Kwa upande wa wanawake, vikundi hivi vimekuwa ni fursa ya ajira na msaada kwenye masuala ya afya, fedha na riziki.

Kwa hakika, wanachama wengi wa vikundi hivi ni wanawake - kati  ya asilimia 58 hadi 64 - hali inayoakisi majukumu ya kijinsia ndani ya jamii (Patino, Mpagalile na Kapingidza, 2025).

Washiriki

Ripoti ya AUC na UNDP ilitokana na utafiti uliofanyika katika mataifa ya Ghana, maeneo ya mpakani ya Liberia-Sierra Leone, Rwanda na Zimbabwe.

Utafiti huo ulihusisha mahojiano na wadau wakuu, visa mikasa, majadiliano ya vikundi lengwa na simulizi za maisha.

Matokeo ya mahojiano yalionesha kuwa sababu kuu ya watu kujiunga na vikundi ni kupata rasilimali za kifedha kwa riba ndogo au bila riba kabisa. Kwa kukatishwa tamaa na mikopo ya benki yenye riba kubwa na masharti ya dhamana, wanajamii wengi hukimbilia vikundi hivi, ambavyo hutoa mikopo nafuu na yenye urahisi wa kupatikana.

Changamoto

Kwa kiasi kikubwa, vikundi hivi vinakosa muendelezo wa kifedha na huwa na changamoto katika ujumuishi.

Suala la ujumuishi limekuwa kama ‘donda ndugu’  linalotokana na ada za uanachama zinazotakiwa kulipwa ili kujiunga na vyama hivi, jambo  linalodhihirisha vikwazo vya kifedha vilivyopo katika jamii.

Aidha, ingawa vikundi hivi vina uwezo mkubwa wa kukabiliana na mishtuko ya mtu mmoja mmoja kama kuugua au kupoteza ajira, hazifanikiwi kukabiliana na changamoto za pamoja kama vile athari za tabianchi na migogoro ya kiuchumi. Hivyo, kutafakari nguvu na udhaifu wa vikundi hivi kunatoa fursa kubwa: mshikamano baina ya vikundi vya kijumuia vya hifadhi ya jamii na sera za hifadhi ya jamii za kitaifa.

Uendeshaji

Vikundi hivi huendeshwa kwa ufanisi mkubwa, hususani kwenye uongozi.

Nchini Liberia na Sierra Leone, asilimia 67 ya vikundi hivi, hufanya uchaguzi wa moja kwa moja wa viongozi wao, ambapo wanawake huwa na asilimia 63 ya nafasi za uongozi nchini Sierra Leone.

Katika suala la usajili rasmi, vikundi vingi huwa na  ushirikiano na mamlaka za serikali za mitaa kama utaratibu wa kiutawala na sio ushirikiano wa kimaudhui. Hivyo, viwango vya usajili hutofautiana sana. Nchini Rwanda, usajili rasmi ni asilimia 100 ukilinganisha na asilimia 45 tu nchini Liberia.

Uwajibikaji na Uaminifu

Ili kuongeza ufanisi wake, vikundi hivi vimeipa suala la uwazi kipaumbele kikubwa.

Vikundi hivi vimejitanabaisha kama taasisi muhimu za kusaidia makundi mbalimbali.

Ni wazi kuwa, mpango wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, ni muhimu katika kusukuma ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususani lengo namba 1.3.

Rwanda kwa mfano, imeonesha ni namna gani jamii zimejengwa kupitia vikundi vya kijumuia kama vile Ubudehe na Umuganda.

Kufikia leo, vikundi hivi vimejidhihirisha kuwa muhimu katika maendeleo ya jamii, tunu na historia.

Mafanikio ya vikundi vya kijumuia vya hifadhi ya jamii hayatoisha hivi karibuni na ni muhimu yakaendelea kuhifadhiwa kupitia mifumo mbalimbali kama: ushirikiano kati ya serikali na jamii; ubunifu wa sera; na ujumuishaji wa mifumo ya kijamii katika sera na programu za kitaifa.

Mwandishi, Esther Mpagalile,  ni mchumi wa kujitegemea anayejikita katika masula ya uchambuzi wa ukuaji jumuishi, tathmini za umaskini, uhifadhi/ ulinzi wa kijamii na utafiti wa sera za kiuchumi.

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi si lazima yaakisi misimamo, mtazamo au sera za uhariri za TRT Afrika.

CHANZO:TRT Afrika