Bara la Afrika linavyopambana na ustawi wa hifadhi ya jamii

Bara la Afrika bado lipo nyuma katika utekelezaji wa sera ya hifadhi ya jamii, ukilinganisha na maeneo mengine ulimwenguni, hali inayowaacha watu wake katika changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

By Esther Mpagalile
Mifuko ya kijamii ina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii za kiafrika./Picha:UNDP

Mchango wa sekta ya hifadhi ya jamii barani Afrika, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, umeendelea kukua maradufu.

Kulingana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, sekta hii imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya watu, hasa kupitia mifuko yake mbalimbali, kama vile mifuko ya afya, uhaliwishaji fedha, ujenzi na mengineyo.

Licha ya jitihada hizi, bado changamoto mbalimbali zikiwemo za hali ya hewa, ufinyu wa bajeti, mazingira ya kisiasa na taasisi dhaifu, zinaendelea kuathiri ufanisi wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Kufikia leo, bara la Afrika bado lipo nyuma katika utekelezaji wa sera ya hifadhi ya jamii, ukilinganisha na maeneo mengine ulimwenguni, hali inayowaacha watu wake katika changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Hii ni kulingana na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

 Makala hii inalenga kuonesha umuhimu wa bara la Afrika kufaidika kupitia mifuko hii.

Kuanzia ngazi za chini

Mifuko ya ngazi ya chini imedhihirisha kuwa suluhisho la kusaidia vikundi vilivyo katika mazingira magumu.

Mifuko hii huundwa na wanachama kuanzia 10 hadi 40, na imekuwa chachu ya mafanikio, hususani kwenye jamii ambazo mifuko mengine imeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Mifuko hii imelinganishwa na kuonekana kushahibiana na ile yenye kuendeshwa kiserikali, hasa katika majukumu yao; licha ya kutofautiana katika wigo namna ya huduma zitolewazo.

Mwishoni mwa mwaka 2025, Tume ya Umoja wa Afrika na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, kwa pamoja, ilizindua mifuko ya aina hii katika mataifa matano, ikilenga kuhudumia jamii 24 na kaya 2,400.

Yatokanayo yanatoa taswira madhubuti yenye kuonesha mustakabali wa mifuko hii barani Afrika.

Upi mchango wa mifuko hii kwa jamii?

Mifuko hii hupokea misaada mbalimbali ikiwemo ya uwezashaji mbalimbali.

Hali kadhalika imekuwa na msaada mkubwa kwa vijana, hasa wanapojiandaa kuoa au kuolewa.

Kwa upande wa wanawake, mifuko hii imekuwa ni fursa ya ajira na kusaidia kwenye nyanja ya afya.

Vivyo hivyo, mifumo hiyo, kwa kiasi kikubwa inaundwa na wanawake, kati ya asilimia 58 hadi 64.

Wahusika wa mifuko hiyo

Ripoti hiyo ya pamoja kati ya Tume ya Umoja wa Afrika na UNDP ilitokana na utafiti uliofanyika katika mataifa kama vile Ghana, Liberia-Sierra Leone, Rwanda na Zimbabwe.

Utafiti huo ulihusisha mahojiano, visa mikasa na majadiliano kwenye vikundi.

Changamoto ya mifumo hiyo

Kwa kiasi kikubwa, mifumo hii inakosa muendelezo wa kifedha, ushirikishwaji na mengineyo.

Suala la ushirikishwaji limekuwa kama ‘donda ndugu’ hususani kwenye ada ya kuingilia, jambo lenye kuonesha changamoto ya kifedha.

Namna ya uendeshaji wa mifuko hiyo

Mifuko huendeshwa kwa ufanisi mkubwa, hususani kwenye uongozi.

Nchini Liberia na Sierra Leone, asilimia 67 ya mifuko hii, hufanya uchaguzi wa moja kwa moja wa viongozi wao, ambapo wanawake huwa na asilimia 63 na nafasi za uongozi nchini Sierra Leone.

 Uwazi wa mifuko hiyo

Ili kuongeza ufanisi wake, mifuko hiyo imeipa suala la uwazi kipaumbele kikubwa.

Mifuko hii ya kijamii imejitanabaisha kama taasisi muhimu za kusaidia makundi mbalimbali.

Ni wazi kuwa, mpango wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, ni muhimu katika kuchagiza ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususani lengo namba 1.3.

Rwanda kwa mfano, imeonesha ni namna gani jamii zimejengwa kupitia mifumo ya ndani kama vile Ubudehe na Umuganda.

Kufikia leo, mifumo imejidhihirisha kuwa muhimu katika maendeleo ya jamii, tunu na historia.

Mafanikio ya mifuko hii haitoisha hivi karibuni na muhimu yakaendelea kuhifadhiwa kupitia maandiko mbalimbali.

Mwandishi wa maoni haya ni mchumi wa kujitegemea anayeangazia masuala ya hifadhi jamii na utafiti wa kiuchumi.