Guinea-Bissau yasitisha jaribio la chanjo ya watoto linalofadhiliwa na serikali ya Trump

Waziri wa Mambo ya Nje Joao Bernardo Vieira alisema kuwa utafiti huo umefungwa, akitaja matatizo yaliyoibuka kutoka kwa jamii ya wanasayansi pamoja na Maseneta wa Marekani.

By
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani kilikubali ruzuku ya dola milioni 1.6 kufadhili mradi huo. / Reuters

Waziri wa Mambo ya Nje wa Guinea-Bissau amesema serikali yake imesitisha jaribio la chanjo ya hepatitis B lililofadhiliwa na utawala wa Trump ambalo Shirika la Afya Duniani liliikosoa kuwa ni kinyume na maadili.

Utafiti huo ulisababisha hasira kutoka kwa wanasayansi na mashirika ya afya ya kimataifa kwa sababu nusu tu ya watoto wachanga katika jaribio hilo wangepewa chanjo mara ya kuzaliwa.

Guinea-Bissau mwezi uliopita ilisimamisha jaribio hilo ikisubiri ukaguzi wa maadili.

Wakosoaji walisema ulitumiwa kupima nadharia zinazohusisha chanjo na usonji, nadharia ambayo Waziri wa Afya wa Marekani Robert F. Kennedy Jr ameipigia debe kwa muda mrefu lakini inapingana na ushahidi wa kisayansi.

Waziri wa Mambo ya Nje Joao Bernardo Vieira alisema katika mahojiano ya Jumanne kwamba utafiti huo umefungwa, akitaja wasiwasi uliotolewa na jamii ya wanasayansi pamoja na seneta za Marekani.

“Haitatokea kabisa,” alisema.

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani kilikubali ruzuku ya dola milioni 1.6 kufadhili mradi huo.

Utafiti huo uliofanywa na watafiti katika Mradi wa Afya wa Bandim ulioko Guinea-Bissau, unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Kusini cha Denmark, ulikusudia kusajili watoto wachanga 14,000, hasa kuchunguza uwezekano wa 'madhara yasiyo maalum' ikiwemo magonjwa ya ngozi na matatizo ya ukuaji wa neva, ikiwa ni pamoja na usonji.

Kulingana na jaribio hilo, nusu ya watoto wachanga wangepewa chanjo mara tu baada ya kuzaliwa, na waliobaki wangepewa baada ya wiki sita, kama ilivyo sasa.

Lakini WHO ilisisitiza wiki iliyopita kwamba utafiti unaotoa tiba iliyothibitishwa kuokoa maisha kwa baadhi lakini si kwa wengine unawaweka watoto wachanga katika "hatari isiyoweza kurekebishika," ilisema.

Ilisema kwamba dozi ya chanjo ya kuzaliwa ya hepatitis B iliyopo sasa ni huduma ya afya ya umma 'inayofaa na muhimu', yenye historia ya ufanisi.

Frederik Schaltz-Buchholzer, mtafiti mkuu, alisema mjadala umebadilika na kuwa wa kisiasa badala ya kuwa wa kisayansi na afya.

“Kila mtu atapata hasara iwapo jaribio hili litasitishwa lakini, zaidi kupoteza imani katika chanjo na utafiti wa afya,” alisema.

Alisema bado kuna matumaini kwamba, pendekezo jipya la jaribio linaweza kukubaliwa siku za usoni.

Mradi wa Bandim umekuwepo kwa miongo kadhaa nchini Guinea-Bissau na watafiti wanasema kazi yao inalenga kuelewa vyema athari kamili za chanjo, zenye faida na hasi.