Kugongwa na nyoka kwa mwanamuziki wa Nigeria Nwangene kwazua mjadala nchini humo
Kifo cha nyota wa Nigeria kimefanya watu waangazie tatizo la kugongwa na nyoka na ukosefu wa huduma za dharura hata maeneo ya mji kama Abuja.
Mwanamuziki mmoja aliyepata umaarufu baada ya kuonekana kwenye The Voice Nigeria 2021 alikuwa amelala katika nyumba yake mjini Abuja mwishoni mwa wiki iliopita, wakati nyoka aina ya swila alipoingia ndani na kumgonga.
Ifunanya Nwangene, 26, alifariki dunia saa chache baada ya tukio hilo. Siyo tu kutoka kwa sumu ya nyoka huyo katika mfumo wake wa damu, lakini katika mfumo mzima wa afya na dharura. Inadaiwa kuwa hospitali ya kwanza aliyopelekwa haikuwa na tiba ya kutoa sumu.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha mfugaji nyoka baadaye akimuondoa nyoka huyo ndani ya nyumba yake huku wakazi wa maeneo hayo wakisema kwa sauti "ni swila!".
Ifunanya ni maarufu kwa miziki ya jazz, na opera. Mwanamuziki huyo, ambaye taaluma yake ni msanifu majengo, alikuwa anajiandaa kwa tamasha la kwanza la peke yake baadaye mwaka huu.
Kifo chake kimefanya raia wa Nigeria kukabiliana na ukweli mchungu: kugongwa na nyoka bado hakuangaziwi kama dharura ya afya ya umma, na kukosekana kwa tiba kunasababisha watu wengi kufariki.
Mtaalamu wa masuala ya nyoka Dkt Abubakar Balla anaamini kuwa kutokupatikana kwa matibabu kumekuwa kukidhoofika miaka na miaka.
"Kugongwa na nyoka ni dharura ya kimatibabu, ilihali hali ya kukosa matibabu inaendelea kuongezeka," Balla ameiambia TRT Afrika. "Suala kuu ni ubora na uhakika wa tiba ya upatikanaji wa tiba ya sumu nchini Nigeria. taifa hilo limekuwa na tiba ya sumu ya nyoka inayoagizwa kutoka India, lakini tiba hiyo imetengenezwa kwa ajili ya nyoka wanaopatikana eneo hilo."
Kutumia tiba ya sumu iliyotengenezwa kwa ajili ya aina tofauti ya nyoka, inadhoofisha matibabu yake, alieleza.
Tatizo la bara zima
Kugongwa na nyoka bado ni tatizo kubwa lakini hakuna taarifa za kutosha Kusini mwa Jangwa la Sahara. Inakadiriwa kuwa watu hadi milioni moja wanagongwa na nyoka kila mwaka katika eneo hilo, huku vifo kati ya 7,000 na 20,000 vikiripotiwa kila mwaka. Kuna changamoto ya kuthibitisha takwimu hizi kutoka na mifumo dhaifu ya kutoa taarifa na matukio ambayo hayafikishwi hospitalini.
Afrika Magharibi pekee, vifo vinavyotokana na kugongwa na nyoka vinakadiriwa kuwa kati ya 3,500 na 5,400 kila mwaka. Katika hospitali moja nchini Nigeria, watu 6,687 waliogongwa na nyoka katika kipindi cha miaka mitatu pekee. Nchini Burkina Faso, kumekuwa na takwimu za watu 114,126 waliogongwa na nyoka katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano (2010–2014), kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Balla anaonya kuwa fikra za kwamba watu wanagongwa na nyoka katika maeneo ya vijijini pekee zinaweza kupotosha.
"Kama tulivyoona tukio baya la Ifunanya, nyoka wanaweza kuingia katika nyumba za mijini," amesema. "Nyumba nyingi za mijini wakati fulani zilikuwa katika maeneo ya misitu. Wakati sehemu zao za kuishi zikiharibiwa au kubadilishwa, nyoka wanaondolewa katika maeneo hayo na kuchanganyana na binadamu. Mabustani ya maua na idadi kubwa ya panya mijini yanavutia nyoka."
WHO imekuwa ikionya kuwa kugongwa na nyoka hakutakiwi kuonekana kama tatizo la afya ambalo halitakiwa kushughulikiwa.
Kwa raia wengi wa Nigeria, kifo cha Ifunanya kimefanya tuwe na mtazamo tofauti kuwa kugongwa na nyoka sio tatizo la vijijini pekee na kudhihirisha ukosefu wa utayari wa kukabiliana na hali ya dharura.