Serikali ya Burundi, ikishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Wakimbizi (UNHCR), siku ya Jumatatu imetangaza mpango wa maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaoishi Burundi kurudi nyumbani kwa hiari huku misaada ikipungua.
Mpango huo, unaotarajiwa kuanza siku ya Alhamisi, ni hatua muhimu katika juhudi za kikanda kutafuta suluhu kwa wakimbizi huku hali ya usalama ikiwa bado tete mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na maafisa.
“Kurudi ni sehemu ya mpango wa hiari, kulingana na matakwa ya kila mtu binafsi,” taarifa ya pamoja ilisema.
Hatua hii inakuja huku kukiwa na uhaba wa misaada wa kukabiliana na idadi kubwa ya wakimbizi.
Mwishoni mwa mwezi Februari, UNHCR ilisema kambi ya wakimbizi ya Busuma ambayo ina raia wa DRC karibu 66,000 waliowasili Burundi tangu mwishoni mwa 2025 inakabiliwa na uhaba wa maji safi, chakula, dawa, makazi na huduma za ulinzi.
Wakisisitiza kuwa hakuna atakayelazimishwa kurudi DRC, mamlaka zimetoa wito kwa wakimbizi wanaotaka kurudi nyumbani kutoa taarifa katika vituo vya kuondokea ili kukamilisha taratibu zifaazo, ikiwemo msaada wa kuwakutahisha watu tena na jamaa zao DRC.
Kipaumbele kitapewa familia zenye watoto wanaosoma, watu wenye mahitaji maalum na maafisa wa serikali.
Kuna wakimbizi 230,000 nchini Burundi, wengi wao wakiwa wanatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kati ya dola milioni $35 zinazohitajika kwa misaada ya wakimbizi nchini Burundi mwaka huu, ni asilimia 20% tu ambayo ilikuwa imepatikana kufikia mwishoni mwa mwezi wa Februari, kulingana na UNHCR.













