Lookman alianza kucheza katika timu ya taifa ya Nigeria tangu 2022 na tangu wakati huo amevaa jezi ya Super Eagles mara 41 na kuifungia magoli 11.
Ademola Lookman Olajade Alade Aylola Lookman alizaliwa 28 iliyopita pale katika maeneo ya Wandsworth, Kusini mwa jiji la London.
Aliwahi kusakata kabumbu akiwa na timu ya vijana ya Charlton Athletic pale England 2014. Mwaka mmoja baadaye akajiunga na timu ya wakubwa ya klabu hiyo.
Aliwakilisha England kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19, 20 na 21 na kwa ujumla alipachika magoli 5 katika mechi zaidi ya 20.
Mwaka 2017 akajiunga na Everton ya Ligi Kuu ya England. Pia alikipiga na RB Leipzig ya Ujerumani.
Miaka miwili baadaye akatinga pale magharibi mwa London akiwa na timu ya Fulham na kisha Leicester.
Ni hapo alipokuwa na Leicester mwaka 2021 ndipo alipowaliza Liverpool alipofungia timu yake goli pekee lilowapa ushindi dhidi ya vijana wa Anfield.
Akiwa Atalanta ya Italia alilaumiwa kwa kukosa penati iliyoifanya timu hiyo kuondolewa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tarehe Mosi mwezi Februari akajiunga na Rojiblancos wa pale jijini Madrid, Atletico kwa mkataba wa miaka minne na nusu.
Siku nne baadaye akajitambulisha alipofunga goli moja katika ushindi wao wa magoli 5-0 dhidi ya Real Betis kwenye michuano ya Copa del Rey.
Ilikuwa ni hatua muhimu katika uchezaji soka wake kwa kuwa alikuwa anatimiza goli la 100. Ademola Lookman mshambuliaji anayeona mbali zaidi ya upeo wake.









