Kiongozi wa kijeshi Guinea atangaza kugombea urais
Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Guinea amewasilisha rasmi jina lake kugombea urais katika uchaguzi wa Disemba, akibatilisha ahadi yake ya awali kwamba hatagombea baada ya kuongoza mapinduzi miaka minne iliyopita.
Jenerali Mamadi Doumbouya, ambaye amekuwa madarakani tangu mapinduzi ya Septemba 2021, anaweza kuendelea kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi kwa miaka mingine saba endapo atashinda uchaguzi uliopangwa kufanyika Disemba 28.
Uchaguzi huo utafanyika chini ya katiba mpya iliyoidhinishwa kupitia kura ya maoni, ambayo inaruhusu wanajeshi wa utawala wa mpito kugombea, na imeongeza kipindi cha urais kutoka miaka 5 hadi 7.
Guinea ni mojawapo ya nchi za Kiafrika, zikiwemo Mali, Niger na Burkina Faso, ambako wanajeshi waliofanya mapinduzi wameimarisha nguvu zao na kukaidi ahadi za awali za kurejea haraka kwa demokrasia.
Muda mfupi baada ya mapinduzi ya Guinea mwaka wa 2021, Doumbouya aliahidi muda wa mpito wenye misingi ya kidemokrasia na kusema kwamba yeye na wanajeshi wengine hawatagombea urais.
Doumbouya anaungana na wagombea wengine wachache katika kinyang'anyiro hicho, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Lansana Kouyaté na Ousmane Kaba, waziri wa zamani wa serikali.
Doumbouya anaripotiwa kukikandamiza chama kikuu cha upinzani, hali inayomuacha katika nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi.
Viongozi wawili wakuu wa upinzani nchini Guinea, Cellou Dalein Diallo na Sidya Toure, wamelazimika kwenda uhamishoni na vyama vyao havitarajiwi kupiga kura mwezi Desemba.
Kiongozi wa junta pia ameunda bodi mpya ya uchaguzi, na amesema wakuu wawili wa taasisi hiyo watateuliwa kwa amri.