Afrika Kusini yampa kifungo cha miaka mitano jela Julius Malema kwa kufyatua risasi

Hakimu alisema Julius Malema amekiuka kwa makusudi sheria za kumiliki silaha kwa kufyatua risasi hewani wakati wa mkutano wa chama cha EFF 2018.

By
Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini Julius Malema akiwa mahamakani mji wa KuGompo, Aprili 16, 2026. / Reuters

Mahakama ya Afrika Kusini imemhukumu kifungo cha miaka mitano gerezani kiongozi wa upinzani Julius Malema siku ya Alhamisi kwa kufyatua risasi katika mkutano miaka minane iliopita.

Mamia ya wanaomuunga mkono kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) wakiwa wamevalia mavazi mekundu walikusanyika nje ya mahakama kusikiliza kifungo hicho.

Makundi ya wanachama wa EFF pia yalikusanyika katika miji mingine, ikiwemo Johannesburg, kufuatilia kesi hiyo kutoka mji wa KuGumpo, zamani ukijulikana kama East London.

Hakimu Twanet Olivier alisema Malema, 45,alikiuka kwa makusudi sheria za kumiliki silaha kwa kufyatua risasi hewani wakati wa mkutano wa chama cha EFF 2018.

"Halikuwa tukio la ghafla," hakimu alisema. "lilikuwa mahsusi kwa jioni hiyo."

"Uamuzi wa kuvunja sheria ulipangwa na kuidhinishwa na mtuhumiwa, na uongozi," alisema.

Upande wa utetezi wa Malema umesema lengo za risasi hizo lilikuwa kusherehekea tu.

Kukata rufaa kwa kifungo

Serikali ilikuwa inataka Malema apewe kifungo cha juu zaidi cha miaka 15 gerezani, alipatikana na hatia mwezi Oktoba. Wanasheria wake wanasema watakata rufaa dhidi ya hukumu na kifungo.

EFF inaseme kesi hiyo ina lengo la kumnyamazisha kiongozi wao huyo. Kwa kifungo hiki, Malema atapoteza nafasi yake ya ubunge. Wanachama wa chama chake wameahidi kuandamana iwapo kiongozi wao atapelekwa gerezani.

Hakimu alisisitiza "siyo chama cha kisiasa kilopatikana na hatia... ni mtu, binafsi."

Chama cha EFF kilishinda chini ya asilimia 10 ya kura katika uchaguzi mkuu wa 2024, na kina wabunge 39 bungeni.