Katika eneo la pwani la Kenya, jamii ya Daida au Dawida, huwa na dansi ya kitamaduni ya kiroho inayoitwa Mwazidika.
Wadawida ni kabila la Kibantu linaloishi hasa katika Kaunti ya Taita-Taveta nchini Kenya.
Dansi ya kiroho ya Mwazidika ni utamaduni unaotumika kukuza ustawi wa mtu binafsi na wa kijamii miongoni mwa kabila la Wadaida.
Ni mchanganyiko wa dansi, muziki, ibada na simulizi ya hadithi.
Mara nyingi hufanyika wakati wa matukio muhimu kama vile ibada za kupita, mavuno, kutawazwa na nyakati za shida kama vile ukame au mafuriko.
Lengo lake ni kuleta ufumbuzi wa matatizo katika jamii hiyo, ulinzi na usawa wa kiroho.
Dansi huanza na ibada inayoitwa 'Kahua', ambapo wazee 12 na vijana hupanda kilima kitakatifu kuwajulisha mababu zao kuhusu tukio.
Ngoma hutengenezwa kutokana na mti mtakatifu, na mimea ya kusafisha huandaliwa.
Kinywaji cha kitamaduni kilichotengenezwa kwa asali na miwa hutolewa kama sadaka kwa mababu.
Dansi hiyo ina ngoma za mdundo, uimbaji na miondoko ambayo inaweza kuwaongoza washiriki katika hali ya kutetemeka.
Mara nyingi inachezwa na wanawake, huku wanaume wakiongoza kupiga ngoma.
Maarifa na ujuzi unaohusiana na tamaduni hiyo hupitishwa wakati huu kupitia mafundisho ya familia na jamii, maonesho na sherehe za kawaida.
Utamaduni huu pia unachukuliwa kama sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuepuka majanga na misiba.
Disemba mwaka 2025, UNESCO iliingiza Mwazindika kwenye Orodha yake ya Urithi wa Utamaduni Usiogusika Unaohitaji Ulinzi wa Haraka, ikitambua umuhimu wake wa kitamaduni na hitaji la kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mila hiyo inakabiliwa na changamoto, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya washiriki na kupungua kwa kasi ya kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
















