Egide Ntakirutimana - mwanariadha anayesukumwa na nidhamu na ari
Egide Ntakarutimana - wanariadha kutoka Burundi / reuters
Egide Ntakirutimana - mwanariadha anayesukumwa na nidhamu na ari
Katika muendelezo wetu wa makala ya wanariadha wa Afrika, safari ya Egide ni ukumbusho kwamba nyuma ya kila ushindi wa kasi kuna hadithi ya nidhamu, kujitolea na azimio thabiti.

Akiwa amezaliwa Burundi mwaka wa 1997, Ntakarutimana amejijengea taaluma kama mwanariadha wa mbio ndefu huku akifanya mazoezi na kushiriki mashindano nchini Italia.

Alianza kujipatia umaarufu katika medani ya kimataifa kwenye Mashindano ya Dunia ya mwaka wa 2022, ambapo alimaliza katika nafasi ya 18 kwenye mbio za mita 10,000.

Tangu wakati huo, ameiwakilisha Burundi katika Mashindano ya Dunia, Mashindano ya Dunia ya mbio za Barabarani, na Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Katika Mashindano ya Dunia ya mbio za Barabarani ya mwaka wa 2023 jijini Riga, alimaliza katika nafasi ya 13 kwenye mbio za kilomita 5.

Na mwaka wa 2024, alishiriki kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki jijini Paris, akishindana katika mbio za mita 5,000.

Hata hivyo, mwaka wa 2026 ndio aliomulikwa tochi zaidi katika taaluma yake.

Ntakarutimana alifungua mwezi Januari kwa ushindi wa mbio za nyika za Campaccio nchini Italia.

Kisha kukafuata mfululizo wa maonyesho ya kuvutia sana uwanjani.

Mnamo mwezi Juni, alikimbia mbio za mita 10,000 kwa muda wa dakika 27 na sekunde 24.59, rekodi yake binafsi aliyokuwa ameiweka awali mwaka wa 2022, kabla ya kuboresha rekodi yake ya mita 3,000 hadi dakika 7 na sekunde 28.13 mnamo mwezi Agosti.

Na mnamo tarehe 5 Septemba, alionyesha kiwango bora zaidi katika taaluma yake hadi sasa.

Akiwa Brussels, Ntakarutimana alikimbia mbio za mita 5,000 kwa muda wa dakika 12 na sekunde 46.73, ikiwa ni rekodi mpya ya taifa la Burundi.

Kiwango hicho kilimweka miongoni mwa wakimbiaji wa kasi zaidi duniani katika mbio za mita 5,000 mwaka wa 2026.

Hivyo, kutoka kuwa mwanariadha kijana wa Burundi hadi kuwa mshiriki wa Olimpiki na sasa mmiliki wa rekodi ya taifa, Egide Ntakarutimana ni mmoja wa wakimbiaji wa mbio ndefu barani Afrika wanaostahili kufuatiliwa kwa karibu.

Ungana nasi TRT Afrika Swahili tunapoibua vipaji vipya na vinavyochipukia katika riadha barani Afrika ambavyo vinastahili kufuatiliwa.

CHANZO:TRT Afrika Swahili