Wachezaji saba wa Eritrea hawajulikani waliko baada ya mechi ya kimataifa

Wachezaji hao hawajulikani waliko tangu mechi yao ya Machi 31, na kocha anaamini kuwa wameenda kujaribu kutafuta fursa za kiuchumi katika mataifa yenye uwezo.

By
Mara ya mwisho kwa Eritrea kucheza katika mechi za barani Afrika ilikuwa 2008. / Wengine

Wachezaji soka saba wa timu ya Eritrea hawajulikani waliko baada ya mechi yao ya kuwania kufuzu kwa AFCON dhidi ya Eswatini wiki iliopita, kocha Hesham Yakan amesema.

Eritrea ilirudi kwa mechi hizo za kuwania kufuzu kwa AFCON mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu 2008, kutokana na kupiga marufuku timu zake kusafiri nje ya nchi baada ya wachezaji wake kadhaa wa timu ya wasiozidi umri wa miaka 20 kukimbia nchini Uganda 2019.

“Wengi wao ni wachezaji wa akiba,” Yakan aliiambia Reuters.

Wachezaji hao hawajulikani waliko tangu mkondo wa pili wa mechi Machi 31, na kocha anasema anaamini watakuwa wameenda kujaribu kutafuta fursa za kiuchumi katika mataifa yenye uwezo.

“Sidhani kama wataendelea kucheza soka,” alisema Yakan, mchezaji wa zamani wa safu ya ulinzi wa Misri aliyecheza katika kikosi cha Kombe la Dunia 1990.

Eritrea ilishinda mkondo wa kwanza 2-0 nchini Morocco, ambapo mechi hiyo ilichezwa kwa kuwa nchi hiyo haina kiwanja kinachokidhi viwango vya Shirikisho la Soka barani Afrika kwa mechi za kimataifa.

Eritrea, ambayo wachezaji wake wanajumuisha kadhaa wanaosakata kabumbu katika vilabu vya Australia, Ujerumani, Norway na Sweden, walimaliza mikondo yote miwili kwa jumla ya ushindi wa 4-1 kwa kuwa waliwafunga Eswatini 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo Machi 31.

Waziri wa Habari wa Eritrea Yemane Gebremeskel hakutaka kuzungumzia suala hilo.

Msemaji wa Shirikisho la Soka la Eritrea pia hakujibu lolote alipotakiwa kutoa tamko.

Wenyeji wa fainali za AFCON 2027 watakuwa Kenya, Tanzania na Uganda.