Makao makuu ya jeshi nchini Iran yametahadharisha kwamba mashambulizi ya Marekani katika maeneo yake ya nyuklia au miundombinu nyeti yatapelekea mashambulizi ya kikanda katika maeneo ya Marekani, pamoja na washirika wanaounga mkono Marekani.
Katika taarifa yake, imesema hatua hiyo itakuwa ni kuongezeka kwa mapigano katika kanda na itakabiliwa vikali na vikosi vyake.
Tahadhari hiyo imekuja baada ya Rais Marekani Donald Trump kutishia kushambulia eneo la nyuklia lililopo chini ya ardhi katika Mlima Pickaxe karibu na kituo cha nyuklia cha Natanz, na kusema Marekani itafanya mashambulizi makali katika eneo hilo.
Amesema anaamini Iran imehamisha mitambo ya nyuklia katika eneo hilo, huku akisema Marekani haina uthibitisho.
Mitambo ya radar imelengwa Kuwait
Awali, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesema vikosi vyake vimeharibu mfumo wa rada wa kutoa ishara ya mapema, karibu na Kambi ya Ali Al Salem na mfumo mwengine wa rada katika kisiwa cha Bubiyan Kuwait katika operesheni ya Nasr 2.
IRGC imesema mifumo ya rada imeharibiwa, na kwamba operesheni za kijeshi zitaendelea.
Marekani imeongeza mashambulizi dhidi ya Iran tangu wiki iliyopita, huku Iran ikirudisha mashambulizi kwa kulenga miundombinu na kambi za Marekani katika nchi kadhaa za eneo hilo.
Mashambulizi kati ya Marekani na Iran yanafanyika licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapiganoi yaliyosimamiwa na Pakistan mwezi Juni.












