Zaidi ya watu 4,500 wamekimbia makazi yao katika majimbo ya Kaskazini mwa Darfur na Blue Nile nchini Sudan kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema.
Kaskazini mwa Darfur, shirika hilo la UN lilisema Jumatano kwamba maafisa wake wanaofuatilia hali ya watu waliolazimika kuhama makazi yao wamekadiria kuwa takriban watu 1,275 walikimbia kutoka vijiji vya Gorbora na Wadi Arkawi, katika eneo la Um Baru, kati ya Septemba 3 na 6.
Familia zilizokimbia makazi yao zilihamia eneo la Karnoy, Kaskazini mwa Darfur, huku baadhi yao wakivuka mpaka na kuingia nchini jirani ya Chad.
IOM imesema hali bado ni “ya wasiwasi na inayobadilika kwa kasi,” na kwamba inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa matukio.
Kwa upande mwingine, shirika hilo limesema takriban watu 3,315, sawa na familia 663, walilazimika kuhama ndani ya siku moja kutoka vijiji kadhaa katika eneo la Geisan, kusini-mashariki mwa jimbo la Blue Nile, kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama.
Uhamaji huo ulirekodiwa Septemba 7 katika vijiji kadhaa, vikiwemo Abu Shneina, Rabaa na Wadi Arab. Familia zilizoathirika zilihamia eneo la Wad al-Mahi, ndani ya jimbo la Blue Nile.
IOM imesema wimbi hilo la hivi karibuni la watu kuhama lilifuatia wimbi jingine lililotokea Septemba 5.
Jumapili, shirika hilo lilisema kuwa watu wengine 1,690 walikuwa wamekimbia makazi yao kutoka vijiji vitatu katika eneo la Kurmuk, Blue Nile, kutokana na kuongezeka kwa ghasia.
Jimbo la Blue Nile limekumbwa na ongezeko la mapigano katika siku za hivi karibuni, huku Kikosi cha RSF na mshirika wake, Sudan People’s Liberation Movement-North (SPLM-N), wakifanya mashambulizi katika maeneo kadhaa.
Mnamo Septemba 4, mamlaka katika eneo la Kurmuk zilisema jeshi la Sudan lilifanikiwa kulizuia shambulio la RSF na SPLM-N katika eneo la Al-Baraka.
Tangu mwishoni mwa Juni, vijiji katika eneo la Um Baru, Kaskazini mwa Darfur, pia vimekabiliwa na mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na RSF. Mashambulizi hayo yamehusisha uvamizi wa masoko, pamoja na kuchomwa na kuporwa kwa vijiji, kwa mujibu wa makundi na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Sudan.
Sudan imekuwa katika vita kati ya jeshi la nchi hiyo na RSF tangu Aprili 2023. Vita hivyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kulazimisha takriban watu milioni 13 kuyakimbia makazi yao, kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa.

















