| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Erdogan kufanya ziara Saudi Arabia atakutana na MBS na Waziri Mkuu wa Pakistan
Ziara ya Rais wa Uturuki Erdogan inafanyika wakati Waziri Mkuu wa Pakistan, akiwa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uhusiano wa mataifa mawili na yanayojiri katika eneo hilo, ikiwemo juhudi za upatanishi kati ya Marekani na Iran.
Erdogan kufanya ziara Saudi Arabia atakutana na MBS na Waziri Mkuu wa Pakistan
Erdogan anatarajiwa kukutana na Mwana Mfalme na Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif. / / AA

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Saudi Arabia siku ya Ijumaa, kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan.

Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran, amesema kuwa wakati wa ziara hiyo Erdogan anatarajiwa kukutana na Mwana Mfalme na Waziri Mkuu wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman (MBS), pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif.

Duran alitoa taarifa hiyo siku ya Alhamisi kupitia NSosyal, mtandao wa kijamii wa Uturuki.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amewasili Saudi Arabia kwa ziara ya siku tatu inayolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili na kujadili maendeleo ya kikanda.

Shirika rasmi la habari la Saudi Arabia (SPA) liliripoti kuwa Sharif alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz mjini Jeddah na Mkuu wa Mkoa wa Makkah, Prince Saud bin Mishaal bin Abdulaziz.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Pakistan (APP), Sharif ameambatana na Mkuu wa Jeshi la Pakistan, Field Marshal Asim Munir, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Ishaq Dar, pamoja na maafisa wengine wakuu wa serikali.

APP ilisema kuwa Sharif anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mohammed bin Salman kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili, pamoja na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa.

Saudi Arabia na Pakistan zina uhusiano wa karibu wa kiulinzi kupitia makubaliano ya pamoja ya ulinzi yaliyosainiwa wakati kukiwa na ongezeko la mvutano katika eneo hilo.

Ziara hiyo inafanyika wakati Islamabad ikiendelea na juhudi za upatanishi kati ya Marekani na Iran.

Mwezi Juni, Qatar ilijiunga na Pakistan katika juhudi za kuzipatanisha Marekani na Iran, hatua iliyosababisha kusainiwa kwa mkataba wa maelewano tarehe 18 Juni na kuanza kwa mazungumzo kuelekea makubaliano ya mwisho.

Hata hivyo, mazungumzo hayo baadaye yalisimama kutokana na kutokubaliana kuhusu masuala ya usalama wa baharini na uhuru wa usafiri katika Mlango-Bahari wa Hormuz. Pamoja na hayo, maafisa kutoka Iran, Oman na Marekani hivi karibuni wameonyesha dalili za maendeleo katika kutatua masuala yaliyosalia.

CHANZO:AA