Wabunge Tanzania waitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na uhaba wa mafuta
Serikali imeshauriwa kuondoa baadhi ya tozo, kupunguza posho na kusitisha vikao visivyo na tija.
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Tanzania wameendelea kuchangia mjadala kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta nchini humo, huku wakitoa mapendekezo mbalimbali ya kupunguza athari kwa wananchi.
Akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amesema ni wakati wa Serikali kuchukua hatua za dharura kupunguza gharama za mafuta. Apendekeza kupunguzwa kwa vikao visivyo vya lazima kwa kipindi cha miezi mitatu pamoja na kuweka ruzuku kwenye mafuta ili kupunguza makali ya bei kwa wananchi.
Aidha, Kingu amesema hatua hizo zitasaidia kuwagusa Watanzania moja kwa moja na kuongeza imani yao kwa Serikali. Pia ameshauri kuondolewa kwa baadhi ya tozo, kupunguzwa kwa posho za Serikali na kusitishwa kwa vikao visivyo na tija.
Kwa upande wake, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, amehoji kauli ya kuwepo kwa mafuta ya kutosha nchini, akitaka kufahamu ni kiongozi gani aliyetoa tamko hilo. Amesema kauli kama hiyo inaweza kuibua mgongano kati ya Serikali, wananchi na wabunge, na kusisitiza kuwa masuala ya mafuta yanapaswa kuzungumzwa na wataalamu kwa uwazi na usahihi.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, amesisitiza umuhimu wa kupunguza gharama za matumizi serikalini na kuimarisha uwajibikaji. Amesema Waziri Mkuu anapaswa kusimamia kikamilifu nidhamu ya matumizi ya Serikali kama mtendaji mkuu, ili kuhakikisha wanaohusika na vitendo vya ufisadi wanachukuliwa hatua stahiki.
Mijadala hiyo inaonesha kuongezeka kwa shinikizo kwa Serikali kuchukua hatua za haraka na za kimkakati katika kukabiliana na changamoto ya mafuta na gharama za maisha kwa ujumla.